Thursday, March 4, 2010

KIKWETE AJIANDIKISHA KUPIGA KURA!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na Mama Salma Kikwete, Jumatano, Machi 3, 2010, wamejiandikisha kama wapiga kura katika kijiji cha kwao cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete waliwasili kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura cha Shule ya Msingi Msoga, kijiji cha Msoga, kiasi cha saa nne asubuhi, na kupokelewa na msimamizi wa kituo hicho, Ndugu Diana Frederick.

Kwenye uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2005, Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete walipiga kura kwenye mji mdogo wa Chalinze wilaya hiyo hiyo ya Bagamoyo lakini zamu hii wameamua kujiandisha, ili waweze kupiga kura kijijini kwao.

Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete wamejiandikisha katika kituo kipya kufuatia kuanza kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura kwa Kanda ya Mashariki.

Uboreshaji wa Daftari la Wapigaji Kura kwa Kanda ya Mashariki ulianza Jumatatu ya wiki hii, Machi Mosi, 2010, na umepangwa kumalizika keshokutwa, Machi 6, 2010.

Chini ya uboreshaji huo, wanaandikishwa wapigaji kura wapya, walioamua kubadilisha vituo vyao vya kupiga kura, ama waliopoteza shahada zao za kupigia kura.

Kufuatia hatua yake hiyo, Rais Kikwete amerudia tena wito wake kwa wananchi wenye sifa za kupiga kura kutumia nafasi ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa kujiandikisha kwa mara ya kwanza kama wapigaji kura, na kwa wale waliopoteza shahada zao kujiandikisha upya, ili wapate sifa za kutumia haki yao ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment