Thursday, March 18, 2010

DODOMA WATAKA RAIS KIKWETE ASIPINGWE!!

Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dodoma, kimetoa tamko la kutaka Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, awe mgombea pekee wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Aidha, katika kumwunga mkono, Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma, kimemchangia Mheshimiwa Kikwete shilingi milioni moja, ili kumwezesha kununulia fomu ya kuomba nafasi hiyo.

Tamko hilo lilifikiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Dodoma kilichofanyika mjini Dodoma Februari 18, mwaka huu, 2010, na limekabidhiwa kwa Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Rais Kikwete, leo mjini Dar es Salaam na ujumbe wa chama hicho.

Ujumbe wa chama hicho Mkoani Dodoma, umeongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa William Kusila, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Adam Kimbisa na Katibu wa chama hicho mkoani humo, Kapteni (mstaafu) John Barongo.

Tamko hilo linasema kuwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete anastahili kuwa mgombea pekee wa Urais kupitia CCM kwa kuzingatia kazi nzuri na utakelezaji wa Ilani ya Uchaguzi chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanywa katika kipindi cha miaka 2005-2010.

Linaongeza tamko hilo: “Rais Kikwete ameonyesha uwezo mkubwa katika kuwaongoza Watanzania, na kuonyesha umakini mkubwa katika utoaji wa maamuzi mbalimbali bila jazba wala woga, chuki au upendeleo kwa Watanzania.”

Akipokea tamko hilo na pesa hiyo, Mheshimiwa Kikwete ameishukuru Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa kumwunga mkono akiahidi kuendelea kukitumikia chama chake na watanzania wote kwa kadri ya uwezo wake.

No comments:

Post a Comment