Thursday, March 4, 2010

MKUTANO WA MKURABITA WAFUNGWA!!!

Katibu Mkuu Ikulu, Bwana Michael Mwanda, amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuuelewa, kuuamini na kuutetea Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na kusimamia vyema utekelezaji wake, ili mpango huo uwakomboe Watanzania kutoka kwenye uchumi usio rasmi kwenda katika uchumi ulio rasmi na unaotambuliwa kisheria.

Katika utekelezaji wa MKURABITA, Bwana Mwanda amewasisitizia Wakurugenzi hao juu ya umuhimu wa kujenga na kuimarisha ushirikiano na kufanya kazi kama timu katika maeneo yao ya kazi ili mpango huo uweze kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.

Bwana Mwanda ameyasema hayo wakati wa kufunga warsha ya siku moja ya Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa iliyofanyika katika ukumbi wa Mtakatifu Gasper mjini Dodoma.

Amewataka Wakurugenzi hao kusimamia vizuri rasilimali chache zilizo chini ya usimamizi wao, wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutoa madaraka yake kwa Serikali za Mitaa (Decentralization by Devolution) ambapo mipango ya kitaifa ukiwemo MKURABITA wenyewe inatarajiwa kuwa kuenezwa (rolled out) kwao.

Aidha Bwana Mwanda amewaomba Wakurugenzi waliohudhuria warsha hiyo kuzingatia umuhimu wa kujifunza miongoni mwao kwa vile tayari katika baadhi ya wilaya kama vile Wilaya ya Mbozi, MKURABITA umeanza kutekelezwa kwa kupima ardhi kwa wanavijiji na mafanikio makubwa kupatikana.

“Hadi sasa wilaya hiyo imewawezesha wananchi kutumia mitaji yao kupata mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 11”, amesema Bwana Mwanda. Amewapongeza viongozi wa wilaya ya Mbozi kwa kazi hiyo nzuri. Vilevile amewashauri Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutembelea Wilaya ya Mbozi na wilaya nyingine ambazo zimepiga hatua katika utekelezaji wa MKURABITA ili waweze kujifunza na kuona mafanikio yaliyopatikana.

Kwa mujibu wa Bwana Mwanda, wilaya nyingine zilizokwisha kuanza utekelezaji wa MKURABITA ni pamoja na Handeni mkoani Tanga, Manispaa ya Kinondoni katika Mkoa wa Dar es Salaam, Kasulu mkoani Kigoma, na Wilaya ya Bagamoyo iliyopo katika Mkoa wa Pwani.

Mada zilizotolewa katika Warsha ya Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ni pamoja na MKURABITA kwa Muhtasari, Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Tatu na ya Nne, Taratibu za Kujenga Mwafaka katika Utekelezaji, na Taratibu za Fedha zinazotumika sasa na matarajio ya baadaye.

No comments:

Post a Comment