Sunday, March 21, 2010

MBINGA WAPATA NEEMA!!!

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii NSSF katika Mkoa wa RUVUMA umekiri kukumbana na ugumu katika uongezaji wa idadi ya waajiri na wanachama wa hiari unaosababisha kupunguza makusanyo ya fedha.

Meneja wa NSSF Mkoani humo WAZIRI NDONDE amesema kumekuwa na mwitikio mdogo hasa kwa wananchi wa hiari licha ya juhudi kubwa zinazofanywa kutangaza manufaa ya wananchi kujiunga katika Mifumo ya Hifadhi za Jamii.

Akizungumza katika Hafla ya kihitimisha Juma la NSSF iliyohudhuriwa na wafanyakazi wa NSSF na Baadhi ya wateja wa Shirika hilo, Bw NDONDE amesema pamoja na kuwepo Changamoto hiyo, katika kipindi cha nusu mwaka zaidi ya shilingi milioni 560 kati ya lengo la shilingi bilioni 1 na milioni 200 zinazotarajiwa kukusanywa Mkoani RUVUMA.

Kuhusu malalamiko ya wanachama wa NSSF kuwa Mfuko huo umekuwa ukitoa mafao kidogo ikilinganishwa na mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii Meneja huyo amesema Serikali inaunda Chombo kitakachodhibiti viwango vya mafao ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Aidha amewaondoa shaka wanachama wa NSSF, kuwa Taarifa za shirika la wafanyakazi la kimataifa ILO zinaonesha kuwa viwango vianvyolipwa na NSSF vitaliwezesha shirika hilo kutoa mafao kwa miaka 50 baadaye ikilinganishwa na mashirika mengine ambayo yanakabiliwa na madeni makubwa (Habari kwa Hisani ya Gerson Msigwa)

Thursday, March 18, 2010

DODOMA WATAKA RAIS KIKWETE ASIPINGWE!!

Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dodoma, kimetoa tamko la kutaka Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, awe mgombea pekee wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Aidha, katika kumwunga mkono, Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma, kimemchangia Mheshimiwa Kikwete shilingi milioni moja, ili kumwezesha kununulia fomu ya kuomba nafasi hiyo.

Tamko hilo lilifikiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Dodoma kilichofanyika mjini Dodoma Februari 18, mwaka huu, 2010, na limekabidhiwa kwa Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Rais Kikwete, leo mjini Dar es Salaam na ujumbe wa chama hicho.

Ujumbe wa chama hicho Mkoani Dodoma, umeongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa William Kusila, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Adam Kimbisa na Katibu wa chama hicho mkoani humo, Kapteni (mstaafu) John Barongo.

Tamko hilo linasema kuwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete anastahili kuwa mgombea pekee wa Urais kupitia CCM kwa kuzingatia kazi nzuri na utakelezaji wa Ilani ya Uchaguzi chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanywa katika kipindi cha miaka 2005-2010.

Linaongeza tamko hilo: “Rais Kikwete ameonyesha uwezo mkubwa katika kuwaongoza Watanzania, na kuonyesha umakini mkubwa katika utoaji wa maamuzi mbalimbali bila jazba wala woga, chuki au upendeleo kwa Watanzania.”

Akipokea tamko hilo na pesa hiyo, Mheshimiwa Kikwete ameishukuru Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa kumwunga mkono akiahidi kuendelea kukitumikia chama chake na watanzania wote kwa kadri ya uwezo wake.

TUCTA WAZIDI KUBANWA!!!!

TAMKO LA SERIKALI JUU YA MGOMO WA TUCTA

Haki iliyotajwa hapo juu imeelezwa bayana katika sura ya saba ya sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004. Kanuni ya utendaji bora na taratibu za kufuatwa katika kutekeleza haki hiyo, imeelekezwa katika sehemu ya nne ya kanuni za utendaji bora toleo la Serikali namba 42 la tarehe 16/02/2007.

Katika sheria iliyotajwa hapo juu kila mfanyakazi anahaki ya kushiriki katika mgomo iwapo kuna mgogoro wa kimaslahi, na kila mwajiri ana haki ya kufungia nje wafanyakazi mahala pa kazi iwapo pana mgogoro wa kimaslahi.

Hata hivyo haki hii imejengewa utaratibu wa kuitekeleza ili kulinda uhai na usalama wa mali, ikiwa ni pamoja na haki za watu wengine ambao pia wana maslahi katika mahusiano hayo. Moja ya mambo yaliyozuiliwa ni kuitisha mgomo unaotokana na malalamiko au haki/ kutotendewa haki.

Kwa kifupi ninachosema ni kwamba mfanyakazi anayohaki ya kugoma kama vile mwajiri alivyo na haki ya kufungia nje mfanyakazi, lakini kwa makundi haya yote mawili ni lazima yazingatie kuwa ipo sheria na zipo kanuni zinazosimamia masuala haya.

Ni muhimu vilevile kufahamu kuwa katika suala la majadiliano baina ya Mwajiri na mfanyakazi wote wanakuwa na haki sawa, hakuna anayeweza kumwamrisha mwenzake, kwa hiyo ni mahala ambapo kila mmoja wao anapaswa kuacha jazba na kuwa na subira. Silaha kubwa ya pande zote mbili ni majadiliano.

KUHUSU TAMKO LA TUCTA LA KUTANGAZA MGOMO TAREHE 5/5/2010
Sisi kama Serikali ni dhahiri tamko hili au kauli hii imetushangaza na pia kiasi Fulani kutusikitisha kwani tunaamini kuwa hali ya mazungumzo ilivyokuwa inaendelea hakukuwa na haja ya kufikia hapo. Kila hoja waliyoieleza Serikali inaifanyia kazi kwa kushirikiana na wao, na wanalijua hilo.

Lakini pamoja na hayo, walipomwandikia barua Kamishna wa Kazi, yenye Ref. TUCTA/AP.15/3/9/2 ya 8/9/2010 kumwarifu juu ya nia yao ya kugoma, sie tulichukua hatua ya kuwajibu na kuwaita Wizarani, ili waje tuzungumze/tujadiliane barua Ref. CAB.360/223/01 ya 11/3/2010 cha kushangaza walikataa na kusema kuwa hawawezi kushiriki katika mazungumzo yoyote kwa sababu wao ni Kamati tu ya Utendaji wakati ambapo azimio la kugoma lilitolewa na Baraza Kuu la TUCTA Ref. TUCTA/P.15/17/5/37 ya 15/3/2010. Kwa bahati nzuri, wakati wanaliandikia barua hiyo ya kukataa kuja tarehe hiyo hiyo waliandika barua LESCO ya kutangaza nia yao ya kugoma ifikapo tarehe 5/5/2010 Ref. TUCTA/M.10/1/2/100 ya 15/3/2010 sababu walizotoa ni kama zifuatazo:-

1. Kutotekeleza mapendekezo ya Tume ya Mishahara ya NTUKAMAZINA ambayo iliteuliwa na Mheshimiwa Rais kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

2. Kutoliangalia swala zima la ukusanyaji wa kodi, hivyo kuwafanya wafanyakazi kuwa eneo kubwa pekee la kulipa kodi za juu wakati wafanyakabiashara wakilipa kodi ndogo na wakati mwingine kukwepa.

3. Wizara ya Kazi kutotangaza maamuzi yake kuhusu mapendekezo ya utafiti uhusuo Vima vya Chini katika sekta binafsi, kinyume na Sheria inavyoagiza.

4. Wizara ya Kazi kushindwa kuunda Bodi mpya za mishahara za Sekta Binafsi tangu zile za zamani zilipomaliza muda wake 1 Aprili 2009.

5. Wizara ya Kazi kushindwa kuitisha vikao vya LESCO ambacho ni chombo cha kuishauri Serikali kuhusu masuala ya wafanyakazi tangu chombo hicho kizinduliwe mwezi Agost 2009 licha ya Rais kuagiza likutane katika kikao chetu cha 4/5/2009 Ikulu Dar es Salaam.

6. Ofisi ya Waziri anayehusika na Menejiment ya Utumishi wa Umma kushindwa kuitisha vikao vya majadiliano yanayohusu maslahi ya Watumishi wa Umma kama sheria ya majadiliano (The Public Service Negotiating Machinery) Act 2003 inavyoagiza.

7. Serikali kutokuwa makini katika kurekebisha malipo dhaifu yatokanayo na Mifuko ya Pensheni ya Wastaafu hivyo kuwafanya Wastaafu wengi kupata mafao duni ya uzeeni.

Kwa kuwa sasa wamefuata mkondo wa sheria unaotakikana kwa kuiandikia LESCO, naamini sasa sheria itachukua mkondo wake katika kutukutanisha pande zote mbili. Sheria inaitaka LESCO kufanya hivyo ndani ya siku 30.

Nina imani hili litafanyika na nina imani pia kuwa ufumbuzi utapatikana kabla ya hiyo tarehe 5/5/2010.

Imesainiwa
Alhaj. Prof. Juma . A. Japuya (Mb)
WAZIRI WA KAZI, AJIRA NA MAENDELEO YA VIJANA

Wednesday, March 17, 2010

CHELSEA YAFA STAMFORD BRIDGE!!


Goli la Mshambuliaji wa Kimataifa wa Cameroon Samuel Etoo Fils limetosha kuwaondosha kwenye Mchuano wa Kombe la Ligi ya Mabingwa Klabu ya Chelsea. Inter Milan ambayo inanolewa na Jose Antonio Mourinho imefanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali kwa jumla ya magoli 3-1.

Tuesday, March 16, 2010

LIVERPOOL YAIUA PORTSMOUTH 4-1!!!



Vijogoo vya Jiji Klabu ya Liverpool vimefanikiwa kuweka kibindoni pointi tatu muhimu baada ya kuifunga Portsmouth maarufu kama Pompey kwa magoli 4-1. Fernando Torres El Nino amesaidia timu yake baada ya kupiga bao mbili!!!

MACHINJONI HAPO (OLD TRAFFORD)!!


Maskani ya Manchester United hayo ambayo yanatambulika kwa jina la Old Trafford Uwanja wenye uwezo wa kuchukua mashabiki zaidi ya elfu sabini na tisa. Timu zetu za hapa nchini nazo zinachangamoto ya kuhakikisha zinakuwa na viwanja kama hivi kwa ajili ya kuongeza mapato yao!!!

Monday, March 15, 2010

MAN UNITED YARUDI KILELENI, MAN CITY YABANWA TENA!!!



Mashetani Wekundu Klabu ya Manchester United imefanikiwa kuichakaza Fulham kwa magoli matatu kwa nunge. Magoli ya Man United yamefungwa na Wayne Rooney ambaye amecheka na nyavu mara mbili huku goli la tatu likifungwa na Dimitry Berbatov. Manchester City wenyewe wameambulia sare ya goli moja kwa moja dhidi ya Sunderland.

BECKHAM HATARINI KUKOSA FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA!!!





Kiungo wa kimataifa wa England David Beckham ambaye anakipiga katika Klabu ya AC Milan huenda akakosa mashindano yake ya nne ya Kombe la Dunia kufuatia kuumia katika mchezo dhidi ya Chievo. Beckham alilazimika kutolewa uwanjani kwa machela baada ya kuumia katika mchezo huo ambao AC Milan imevuna uhsindi wa goli moja kwa nunge. Kiungo huyo anatarajiwa kupelekwa Finland kufanyiwa upasuaji kwa madaktari bingwa.

Sunday, March 14, 2010

LANGA LANGA YAANZA KWA KASI!!!


Driver Race Time
1 Spain F Alonso 1:39:20.396
2 Brazil F Massa 1:39:36.495
3 Great Britain L Hamilton 1:39:43.578
4 Germany S Vettel 1:39:59.195
5 Germany N Rosberg 1:40:00.609
6 Germany M Schumacher 1:40:04.559
7 Great Britain J Button 1:40:05.676
8 Australia M Webber 1:40:06.756
9 Italy V Liuzzi 1:40:13.404
10 Brazil R Barrichello 1:40:22.885
Mashindano ya kwanza ya Msimu wa Formula One maarufu kama Langa Langa umeanza na kushuhudia Fernando Alonso akiibuka kidedea katika Behrain Grand Prix. Huku mkongwe Michael Schumacher ambaye ni bingwa mara saba liyerejea tena katika mchuano akiangukia nafasi ya sita.

PACQUIAO AMCHAKAZA CLOTTEY!!!


Bingwa wa WBO Manny Pacquiao amefanikiwa kutetea taji lake baada ya kumchakaza Bondia wa Ghana Joshua Clottey kwa pointi baada ya raundi kumi na mbili kumalizika bila ya kuwepo mbabe!!

Friday, March 12, 2010

NIPO MZIGONI!!!


Siku moja moja na me niking'aa sharubu si mbaya sana. Hapa nilikuwa narekodi kipindi cha Mwanamichezo wa Wiki ambacho kinarushwa kupitia Mlimani Tv ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam. Kipindi hiki kinaruka Jumamosi saa kumi na nusu hadi kumi na moja. Marudio ni siku ya Jumapili kuanzia saa moja usiku hadi moja na nusu.

VIJANA WAKICHAKARIKA KUSAKA MKATE WA SIKU!!!





Shughuli hizi zimekuwa maarufu sana hivi sasa kutokana na vijana wengi kujikita katika kusafisha kucha kina dada na kujipatia riziki. Haikuwa mazoea kwa wanaume kuwasafisha miguu kinadada lakini hali ngumu ya maisha inawafanya vijana wawe wabunifu kila kukicha.

UWEKEZAJI WA RITES MATATANI!!!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Baraza la Mawaziri Ijumaa, Machi 12, 2010, katika kikao chake kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam, chini ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limejadili hali ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kufanya maamuzi ya msingi kwa kukubaliana kama ifuatavyo:

•Kwamba Serikali ianze mara moja kujadiliana na RITES, mbia wa Serikali katika kampuni ya TRL, kwa lengo la Serikali kununua hisa 51 za RITES katika kampuni hiyo. Kwa sasa RITES inamiliki asilimia 51 na Serikali inamiliki asilimia 49 katika TRL.

•Kwamba baada ya hapo, Serikali itafanya matayarisho ya msingi ikiwa ni pamoja na kurekebisha kasoro na kuangalia mustakabali wa TRL, na kuiandaa kampuni hiyo kwa ajili ya kutafutiwa mbia mwingine wa kushirikiana na Serikali katika kuendesha TRL.

BARABARA YA SONGEA-NAMTUMBO KUJENGWA!!

Waziri wa Miundombinu Daktari Shukuru Jumanne Kawambwa amewaahidi wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuwa Ujenzi wa barabara za SONGEA – NAMTUMBO na PERAMIHO – MBINGA zenye jumla ya kilometa 140 kwa kiwango cha lami utaanza kabla ya Mwezi Juni Mwaka huu.

Daktari Kawambwa aliyekuwa katika ziara ya siku tatu Mkoani RUVUMA kwa lengo la kukagua miundombinu ya barabara, Gati ya Bandari ya Mbambabay na Kivuko cha Mto RUHUHU amesema hivi sasa Serikali inakamilisha taratibu za mwisho za kuwapata wakandalasi ambao wataanza kazi mwezi Mei.

Akiwa katika ziara hiyo Wananchi katika maeneo tofautitofauti wameonesha kuwa na mashaka na kauli hiyo ya Ukweli wa Kuanza kwa ujenzi wa Lami, na mara zote ilimlazimu Daktari Kawambwa kuwaondoa shaka kuwa Jambo hilo sio Propaganda na wala halina uhusiano na Uchaguzi Mkuu Ujao.

Hata hivyo akiwa njiani Waziri wa Miundombinu amekutana na Changamoto ya gari lake aina Toyota Landcruiser VX V8 kukwama barabarani kutokana na Mvua nyingi na Ubovu Mkubwa wa barabara za SONGEA – MBAMBABAY na SONGEA – TUNDURU ambazo zinasababisha magari mengi kukwama.

Kabla ya kuondoka Mkoani RUVUMA Daktari Kawambwa pia ametembelea kiwanja cha Ndege cha SONGEA ambapo ameelezwa kuwa hakuna safari za ndege za abiria zinazofanyika kupitia kiwanja hicho kutokana na kukosa mafuta ya ndege na Maji, na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa RUVUMA kuendelea kufuatilia uwepo wa mafuta ya ndege na kuhakikisha watu waliovamia kiwanja hicho wanaondolewa. (Habari kwa Hisani ya Gerson Msigwa)

HAGREAVES KUCHELEWA KUREJEA UGANI!!


Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amethibitisha kuchelewa kurejea ugani kwa kiungo wake Owen Hagreaves ambaye amekuwa akisumbuliwa na maaumizu kwa muda mrefu.Owen atachelewa kurejea baada ya kujitonesha maumivu aliyokuwa nayo katika mchezo wa kirafiki wa wachezaji wa akiba.

DROGBA MCHEZAJI BORA WA AFRIKA!!!


Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tembo wa Afrika, Ivory Coast ambaye anakipiga katika klabu ya Chelsea, Didier Drogba ameibuka mchezaji bora wa mwaka na kuwabwaga Samuel Etoo (Cameroon) na Michael Essien (Ghana). TP Mazembe ni Klabu bora barani wakati Tresor Mputu naye akichukua tuzo ya uchezaji bora kwa wale ambao wanacheza ligi ya ndani. Algeria ni timu bora kwa ngazi ya timu ya Taifa wakati Masabiki wa Afrika Kusini, Bafana Bafana wakiwa na mavuvuzela yao wametajwa kama bora kwenye ushangiliaji.

Thursday, March 4, 2010

MZUNGU AKIWA KATIKA SAGURA SAGURA!!!!!





Jamani hii nchi ina raha sana na ndiyo maana kila mmoja anakuwa na uhuru wa kufanya chochote. Huyu mzungu naye anasaka viwalo vyake hapo!!!

MKUTANO WA MKURABITA WAFUNGWA!!!

Katibu Mkuu Ikulu, Bwana Michael Mwanda, amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuuelewa, kuuamini na kuutetea Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na kusimamia vyema utekelezaji wake, ili mpango huo uwakomboe Watanzania kutoka kwenye uchumi usio rasmi kwenda katika uchumi ulio rasmi na unaotambuliwa kisheria.

Katika utekelezaji wa MKURABITA, Bwana Mwanda amewasisitizia Wakurugenzi hao juu ya umuhimu wa kujenga na kuimarisha ushirikiano na kufanya kazi kama timu katika maeneo yao ya kazi ili mpango huo uweze kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.

Bwana Mwanda ameyasema hayo wakati wa kufunga warsha ya siku moja ya Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa iliyofanyika katika ukumbi wa Mtakatifu Gasper mjini Dodoma.

Amewataka Wakurugenzi hao kusimamia vizuri rasilimali chache zilizo chini ya usimamizi wao, wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutoa madaraka yake kwa Serikali za Mitaa (Decentralization by Devolution) ambapo mipango ya kitaifa ukiwemo MKURABITA wenyewe inatarajiwa kuwa kuenezwa (rolled out) kwao.

Aidha Bwana Mwanda amewaomba Wakurugenzi waliohudhuria warsha hiyo kuzingatia umuhimu wa kujifunza miongoni mwao kwa vile tayari katika baadhi ya wilaya kama vile Wilaya ya Mbozi, MKURABITA umeanza kutekelezwa kwa kupima ardhi kwa wanavijiji na mafanikio makubwa kupatikana.

“Hadi sasa wilaya hiyo imewawezesha wananchi kutumia mitaji yao kupata mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 11”, amesema Bwana Mwanda. Amewapongeza viongozi wa wilaya ya Mbozi kwa kazi hiyo nzuri. Vilevile amewashauri Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutembelea Wilaya ya Mbozi na wilaya nyingine ambazo zimepiga hatua katika utekelezaji wa MKURABITA ili waweze kujifunza na kuona mafanikio yaliyopatikana.

Kwa mujibu wa Bwana Mwanda, wilaya nyingine zilizokwisha kuanza utekelezaji wa MKURABITA ni pamoja na Handeni mkoani Tanga, Manispaa ya Kinondoni katika Mkoa wa Dar es Salaam, Kasulu mkoani Kigoma, na Wilaya ya Bagamoyo iliyopo katika Mkoa wa Pwani.

Mada zilizotolewa katika Warsha ya Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ni pamoja na MKURABITA kwa Muhtasari, Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Tatu na ya Nne, Taratibu za Kujenga Mwafaka katika Utekelezaji, na Taratibu za Fedha zinazotumika sasa na matarajio ya baadaye.

KIKWETE AJIANDIKISHA KUPIGA KURA!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na Mama Salma Kikwete, Jumatano, Machi 3, 2010, wamejiandikisha kama wapiga kura katika kijiji cha kwao cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete waliwasili kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura cha Shule ya Msingi Msoga, kijiji cha Msoga, kiasi cha saa nne asubuhi, na kupokelewa na msimamizi wa kituo hicho, Ndugu Diana Frederick.

Kwenye uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2005, Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete walipiga kura kwenye mji mdogo wa Chalinze wilaya hiyo hiyo ya Bagamoyo lakini zamu hii wameamua kujiandisha, ili waweze kupiga kura kijijini kwao.

Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete wamejiandikisha katika kituo kipya kufuatia kuanza kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura kwa Kanda ya Mashariki.

Uboreshaji wa Daftari la Wapigaji Kura kwa Kanda ya Mashariki ulianza Jumatatu ya wiki hii, Machi Mosi, 2010, na umepangwa kumalizika keshokutwa, Machi 6, 2010.

Chini ya uboreshaji huo, wanaandikishwa wapigaji kura wapya, walioamua kubadilisha vituo vyao vya kupiga kura, ama waliopoteza shahada zao za kupigia kura.

Kufuatia hatua yake hiyo, Rais Kikwete amerudia tena wito wake kwa wananchi wenye sifa za kupiga kura kutumia nafasi ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa kujiandikisha kwa mara ya kwanza kama wapigaji kura, na kwa wale waliopoteza shahada zao kujiandikisha upya, ili wapate sifa za kutumia haki yao ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

VITUO VYA KUPIGIA KURA VYASHAMBULIWA IRAQ!!


Zoezi la Kupiga kura kuchagua wabunge nchini Iraq limeingia dosari baada ya kushambuliwa na kusababisha vifo vya watu kumi na nne. Washambuliaji wa kujitoa mhanga wameshambulia vituo viwili vya kupigia kura katika siku ya kwanza ya Uchaguzi wa Wabunge!!

HASHEEM AZUA MJADALA DUNIANI!!!


Mchezaji wa Mpira wa Kikapu kutoka Tanzania, Hasheem Thabeet amezua mjadala katika mitandao mbalimbali duniani kutoka na hatua ya kushushwa kutoka NBA kwa kile ambacho kinaelezwa ni kushindwa kufikia kiwango alichotarajiwa. Mchezaji huyo wa Memphis Grizzlies amepelkwa timu ya Dakota kwa ajili ya kupandisha kiwango chake. Kila la kheri Hasheem usikate tamaa na hiyo ndiyo iwe chanzo chako cha kurejea NBA kwa nguvu!!!

Wednesday, March 3, 2010

TTC SONGEA MAMBO SI SHWARI!!!

Kikao cha Bodi ya Chuo cha Ualimu SONGEA kilichofanyika jumatano kwa siku nzima kimeshindwa kutoa hatma ya Mawaziri 10 wa serikali ya wananchuo waliosimamishwa masomo tangu mwishoni mwa mwezi NOVEMBER mwaka jana kwa madai ya kuchochea mgomo wa wachuo waliokuwa wakimpinga mwalimu wa maadili wa chuo hicho kuwavua madaraka mawaziri waliowachagua na kuwateua anaowataka yeye.

Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Chuo hicho ambaye ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa RUVUMA DR ANSERM TARIMO, ameonekana kugongana kimaelezo na Mkuu wa Chuo hicho MPELI MBOSA juu ya Sakata wakati wakihojiwa na waandishi wa habari.

DR TARIMO amesema Hatma ya wananchuo hao bado haijapatikana na kusisitiza ni lazima itafutwe haki kwanza, wakati Mkuu wa Chuo MPELI MBOSA amedai hatambui chochote kilichotokea wala Mkutano wa Maridhiano uliofanyika Octoba 27 mwaka jana na kutoa suluhu ambapo Mwalimu wa maadili wa Chuo hicho VALENTINE MAYAYA aliomba radhi kwa kuwa chanzo cha tatizo.

Kuhusu hatma ya wanafunzi waliosimamishwa ambao wanaendelea kuhangaika mjini SONGEA wakisubiri hatma yao Bw MBOSA amesema hilo halimhusu. (Taarifa kwa hisani ya Gerson Msigwa)

ENGLAND YAIZAMISHA MISRI!!!






Mabingwa wa Afrika, Misri maarufu kama Mapharao wamekumbana na kichapo kutoka kwa timu ya taifa ya England katika mchezo uliopigwa katika dimba la Wembley. Magoli mawili ya Peter Crouch moja la Shaun Wright Philipps walitosha kulizima lile lililofungwa na Mohamed Zidan na kufanya mambo kuwa 3-0