Tuesday, April 5, 2011

UN YAMWAGA SIFA KWA UONGOZI WA AWAMU YA NNE!!

Umoja wa Mataifa (UN) umeipongeza Serikali ya Tanzania na uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa mafanikio makubwa ya kupunguza vifo vya vitoto vichanga vinavyozaliwa na ugonjwa wa ukimwi na pia kupunguza vifo vya akinamama wajawazito kutokana na ugonjwa huo.

Umoja huo umesema kuwa kwa kasi ya sasa inawezekana Tanzania ikamaliza kabisa vifo vya watoto kutokana na ugonjwa huo katika miaka mitatu minne kama hali haitabadilika kwa namna yoyote ile.

Aidha, Umoja huo umemwomba Rais Kikwete kuongoza kampeni ya kutaka uhamisho wa teknolojia ya kutengeneza na kuzalisha dawa za kurefusha maisha ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kutoka nchi tajiri ili zizalishwe katika nchi zinazoendelea.

Pongezi hizo kwa Tanzania na kwa uongozi wa Rais Kikwete zimetolewa Jumatatu, Aprili 4, 2011, na Naibu Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Asha Rose Migiro, akifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukimwi la Umoja wa Mataifa (UNAIDS), Mheshimiwa Michel Sidibe, wakati walipokutana na Rais Kikwete Ikulu, Dar es Salaam.

“Tunatambua na kuthamini sana maendeleo makubwa yaliyopatikana katika Tanzania chini ya uongozi wa Serikali katika utekelezaji wa Lengo la Sita la Maendeleo ya Milenia (MDG). Umepunguza vifo vya vichanga vinavyozaliwa na virusi vya ukimwi hadi kufikia watoto saba tu kila siku na katika miaka mitatu ama minne mnaweza kabisa kufikia ziro,” amesema Mama Asha Rose Migiro ambaye ameongoza ujumbe wa UN kuja kumwona Rais Kikwete.

MDG ya sita inaelekeza kupambana na ukimwi, malaria na maradhi mengine duniani na lengo ni kupunguza vifo kutokana na magonjwa hayo kwa angalau nusu, kusimamisha kuenea kwa magonjwa na kuanza kubadilisha mwelekeo wa magonjwa hayo ifikapo mwaka 2015.

Ameongeza Mama Migiro ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya UN:

“Tanzania, chini ya uongozi wako, imepata mafanikio makubwa sana katika kupunguza maambukizi, kujali na kutunza waathirika na kuwapatia dawa za kurefusha maisha yao. Uongozi wako katika hili umekuwa imara na mzuri sana.”

Naye Mheshimiwa Sidibe amemwomba Rais Kikwete kuongoza kampeni ya kuhakikisha kuwa dawa za viwango vyote vya kupambana na ukimwi zinaanza kutengenezwa na kuzalishwa katika nchi zinazoendelea badala ya kutengenezwa katika nchi tajiri zinazoweka masharti makubwa katika kuruhusu dawa hizo kutengenezwa kwa bei rahisi zaidi katika nchi masikini.

“Mheshimiwa Rais tunakuomba uwe sauti yetu, tunakuomba uongoze msukumo mpya wa kutaka nchi masikini nazo ziwe na teknolojia ya kutengenezwa dawa bora zaidi za kukabiliana na ukimwi. Kama hatutaweza kuzizalisha dawa hizi kwenye nchi zetu itafikia mahali hata watu milioni tano wanapata dawa hizo katika Afrika wakajikuta hawapati dawa siku moja,” Mheshimiwa Sidibe amemwambia Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment