Wednesday, April 27, 2011

MAKATIBU NA MANAIBU MAKATIBU WAPYA WATAJWA!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa Katibu Mkuu mmoja wa Wizara, na Naibu Makatibu Wakuu 10 wa Wizara mbalimbali.

Aidha, Rais Kikwete amemhamisha Naibu Katibu Mkuu mmoja kutoka Wizara moja kwenda nyingine.

Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam, leo, Jumatano, Aprili 27, 2011, na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi Bwana George Yambesi inasema kuwa uteuzi huo wa maofisa hao waandamizi wa Serikali unaanzia Alhamisi iliyopita, Aprili 21, mwaka huu, 2011, na wataapishwa Jumamosi wiki hii, Aprili 30, saa sita mchana.

Taarifa hiyo inasema kuwa katika uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bwana Job D. Masima kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Aidha, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemhamisha Injinia Mbogo Futakamba aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji kwenda Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Taarifa hiyo inasema kuwa Naibu Makatibu Wakuu walioteuliwa na Mheshimiwa Rais ni kama ifuatavyo:

* Bwana Aphayo Kidata ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ikulu. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Kidata alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

* Bwana Hab Mkwizu ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Mkwizu alikuwa Karani wa Baraza la Mawaziri.

* Bwana Charles Amos Pallangyo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Pallangyo alikuwa Mkurugenzi wa Uratibu – Ofisi ya Waziri Mkuu.

* Bibi Mwamini Juma Malemi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kabla ya hapo alikuwa Msaidizi wa Makamu wa Rais katika masuala ya Maendeleo ya Jamii na Uratibu wa Malalamiko ya Jamii na Uratibu wa Malalamiko ya Wananchi.

* Injinia Mussa Ibrahim Iyombe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Ulinzi na JKT. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Miundombinu ya Usafiri katika Wizara ya Ujenzi.

* Injinia Dkt. John Stanslaus Ndunguru ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Ujenzi. Kabla ya hapo, alikuwa Mkurugenzi wa Huduma na Ufundi katika wizara hiyo hiyo ya Ujenzi.

* Bwana John Thomas James Mngodo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Uchukuzi. Kabla ya uteuzi wake alikuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula.

* Bibi Anna T. Maembe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Kabla ya uteuzi wake, Bibi Maembe alikuwa Mkurugenzi wa Mazingira na Habari wa NEMC.

* Bibi Sihaba Nkinga ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Uchukuzi.

* Injinia Bashir J. Mrindoko ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Maji. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Mrindoko alikuwa Kamishna wa Nishati na Mafuta ya Petroli.

CLEMENT MSHANA MKURUGENZI MPYA TBC!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Clement Senzota Mwete Mshana kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam, leo, Jumatano, Aprili 27, 2011, na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana George Yambesi inasema kuwa uteuzi huo unaanzia Alhamisi iliyopita, Aprili 21, mwaka huu, 2011.

Kabla ya uteuzi huo, Bwana Clement Senzota Mwete Mshana alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo).

Bwana Mshana anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bwana Dunstun Tido Mhando ambaye amemaliza muda wake wa utumishi kwa mujibu wa mkataba wake.

Thursday, April 21, 2011

RAIS KIKWETE AKUTANA NA VIONGOZI WA WAFANYAKAZI IKULU!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Jumatano, Aprili 20, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini.

Mkutano huo wa kawaida kati ya Rais Kikwete na vikundi mbalimbali vya jamii kikiwemo kile cha viongozi wa wafanyakazi umefanyika Ikulu, Dar es Salaam katika mazingira ya kuelewana.

Mkutano huo umechukua kiasi cha saa tano na kuhudhuriwa na viongozi 20 wa wafanyakazi, mawaziri wanaohusika na masuala na haki za wafanyakazi na watumishi wengine waandamizi wa Serikali.

Viongozi wao wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bwana Ayoub Omar Jumaa umeshirikisha viongozi kutoka TUCTA yenyewe, Chama cha Walimu Tanzania (CWT), TPWU, TEWUTA, DOWUTA, TRAWU, CHODAWU, TUICO, TASU, TAMICO TUGHE na COTWU.

Mawaziri waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Kazi na Ajira, Mheshimiwa Gaudencia M. Kabaka, Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma, Mheshimiwa Hawa A. Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Mheshimiwa George Huruma Mkuchika.

Katika kikao hicho, pande hizo mbili zimejadili masuala mengi yanayohusu haki na maslahi ya wafanyakazi na masuala mengine muhimu ya taifa yakiwamo madai ya malimbikizo ya malipo ya wafanyakazi ikiwamo mishahara.

Rais Kikwete na viongozi hao pia wamejadili kuhusu uwezekano wa Serikali kuongeza mishahara ya watumishi kwa kuzingatia upandaji wa gharama za maisha, uwakilishi wa wafanyakazi katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na uwezekano wa Serikali kupunguza kodi kwa wananchi ili kutoa ahueni zaidi ya maisha kwa wananchi.

Kuhusu sera ya Serikali ya kupunguza kodi ili kutoa ahueni ya maisha kwa wananchi, Rais Kikwete amewaambia viongozi hao wafanyakazi: “Hili tulikwishakubaliana kuwa lazima tuchukue hatua za mara kwa mara kuongeza unafuu wa maisha kwa wananchi wetu. Tutaendelea nalo hili kwa sababu ni muhimu sana. Suala kubwa hapa ni kutekeleza sera ya kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi. Lazima tufanye kila liwezekanalo kufanikisha hili.”

Kuhusu ombi la viongozi hao kuwa Serikali itoe dhamana kwa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ili kuliwezesha shirika kuwa na uwezo wa kukopa fedha katika mabenki kusaidia kuliimarisha, Rais Kikwete ameigiza Wizara ya Fedha kuchukua hatua za haraka kuhakikisha hili linafanikiwa. “Tulifanye hili haraka sana, halina sababu ya kucheleweshwa kwa sababu TTCL ni shirika muhimu sana.”

WENGER HAJAKATA TAMAA YA UBINGWA WAKATI CHELSEA IKICHUKUA NAFASI YA PILI!!




Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger a,esema wataendelea kupigia Ubingwa hadi hatua mwisho licha ya kuambulia sare ya magoli 3-3 dhidi ya Tottenham Hotspurs!!! Mabingwa Watetezi Chelsea wamejikita katika nafasi ya Pili baada ya ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Birmingham City!!

MADRID MABINGWA WA COPA DEL REY KWA KUIFUNGA BARCELONA!!





Goli la Kichwa lililofungwa na Cristiano Ronaldo katika mchezo wa Fainal ya Kombe la Mfalme nchini Sapin lilitosha kuwapa Ubingwa Real Madrid na kuwanyang'anya taji Barcelona!! Goli hilo lilifungwa katika muda wa nyongeza za dakika thelathini baada ya dakika tisini timu hizo kutoshana nguvu!!

Wednesday, April 13, 2011

INTER MILAN WATEMA KOMBE, MADRID WAKIWAFUATA BARCELONA!!






Mabingwa Watetezi wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, Inter Milan jana wameondolewa kwenye mashindano baada ya kukubali kichapo kutoka kwa Schalke 04 kwa magoli 2-1!! Real madrid wenye wametinga nusu fainal baada ya kuwafunga Tottenham Hotspurs kwa goli 1-0!!

Tuesday, April 12, 2011

MANCHESTER UNITED YAZIMA NDOTO ZA CHELSEA!!







Ndoto za Chelsea kufuzu kwenye Nusu Fainal ya Ligi ya Mabingwa Bara Ulaya zimeyeyuka kwenye Uwanja wa Old Traford baada ya kukubali kipigo kingine cha magoli 2-1 kutoka Manchester United!! Kwa matokeo hayo Chelsea hawana chao kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya Msimu huu baada ya kuondoshwa kwenye mashindano!!

Monday, April 11, 2011

MAN CITY MAJI YAZIDI UNGA MBELE YA LIVERPOOL!!




Klabu ya Liverpool, Vijogoo Vya Jiji jana walifanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa magoli 3-0 mbele ya Manchester City ikiwa ni kulipiza kisasi cha mchezo wa kwanza!! Ushindi huo umerejesha matumaini kwa Liverpool kufanya vizuri kwenye michezo iliyobakia!!!

Wednesday, April 6, 2011

MAN UTD, BARCELONA ZAWEKA HAI MATUMAINI YA KUTINGA NUSU FAINAL!!








Goli la pekee la Mshambuliaji wa Kimataifa wa Uingereza Wayne Rooney limetosha kuwapa ushindi wa ugenini Manchester United katika mchezo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya mbele ya Chelsea. Barcelona kwa upande wao wametoa kipigo kizito kwa Shakhtar Donetsk cha magoli 5-1!!!

INTER MILAN, TOTTENHAM WASHIKWA PABAYA LIGI YA MABINGWA!!





Mabingwa Watetezi wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya Inter Milan imeanza vibaya hatua ya Robo Fainal baada ya kupata kichapo kutoka kwa Schalke 04 wakiwa San Siro baada ya kufungwa magoli 5-2 huku Real Madrid wakitumia vyema Uwanja wa nyumbani kwa kuifunga Tottenham Hotspurs kwa magoli 4-0!!

RWEGASIRA WA TRAWU KUZIKWA LEO IKULU YATUMA RAMBIRAMBI!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Omar Nundu kufuatia kifo cha ghafla cha Sylvester Rwegasira, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU) kilichotokea tarehe 4 Aprili, 2011 kutokana na maradhi ya moyo.

Rais Kikwete amesema kuwa kifo cha Sylvester Rwegasira kimeleta simanzi kubwa siyo kwa familia yake tu, bali pia jumuiya ya wafanyakazi hapa nchini kwani Marehemu Sylvester alikuwa mtetezi mkubwa wa wafanyakazi hususan wale wa Reli ambao yeye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama chao, kwani alijitoa kwa moyo wake wote kutetea maslahi yao.

Kupitia kwa Waziri wa Uchukuzi, Rais Kikwete ametoa pole nyingi kwa familia ya Marehemu Sylvester Rwegasira kwa kupotelewa na kiongozi muhimu wa familia, hivyo anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke mahali pema peponi roho ya Marehemu Rwegasira.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amewaomba wanafamilia ya Marehemu Rwegasira kuwa watulivu, wavumilivu na wenye subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao, huku akiwahakikishia kuwa yeye binafsi yuko pamoja nao katika muda wote wa maombolezo ya Marehemu Sylvester Rwegasira.

Tuesday, April 5, 2011

UN YAMWAGA SIFA KWA UONGOZI WA AWAMU YA NNE!!

Umoja wa Mataifa (UN) umeipongeza Serikali ya Tanzania na uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa mafanikio makubwa ya kupunguza vifo vya vitoto vichanga vinavyozaliwa na ugonjwa wa ukimwi na pia kupunguza vifo vya akinamama wajawazito kutokana na ugonjwa huo.

Umoja huo umesema kuwa kwa kasi ya sasa inawezekana Tanzania ikamaliza kabisa vifo vya watoto kutokana na ugonjwa huo katika miaka mitatu minne kama hali haitabadilika kwa namna yoyote ile.

Aidha, Umoja huo umemwomba Rais Kikwete kuongoza kampeni ya kutaka uhamisho wa teknolojia ya kutengeneza na kuzalisha dawa za kurefusha maisha ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kutoka nchi tajiri ili zizalishwe katika nchi zinazoendelea.

Pongezi hizo kwa Tanzania na kwa uongozi wa Rais Kikwete zimetolewa Jumatatu, Aprili 4, 2011, na Naibu Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Asha Rose Migiro, akifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukimwi la Umoja wa Mataifa (UNAIDS), Mheshimiwa Michel Sidibe, wakati walipokutana na Rais Kikwete Ikulu, Dar es Salaam.

“Tunatambua na kuthamini sana maendeleo makubwa yaliyopatikana katika Tanzania chini ya uongozi wa Serikali katika utekelezaji wa Lengo la Sita la Maendeleo ya Milenia (MDG). Umepunguza vifo vya vichanga vinavyozaliwa na virusi vya ukimwi hadi kufikia watoto saba tu kila siku na katika miaka mitatu ama minne mnaweza kabisa kufikia ziro,” amesema Mama Asha Rose Migiro ambaye ameongoza ujumbe wa UN kuja kumwona Rais Kikwete.

MDG ya sita inaelekeza kupambana na ukimwi, malaria na maradhi mengine duniani na lengo ni kupunguza vifo kutokana na magonjwa hayo kwa angalau nusu, kusimamisha kuenea kwa magonjwa na kuanza kubadilisha mwelekeo wa magonjwa hayo ifikapo mwaka 2015.

Ameongeza Mama Migiro ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya UN:

“Tanzania, chini ya uongozi wako, imepata mafanikio makubwa sana katika kupunguza maambukizi, kujali na kutunza waathirika na kuwapatia dawa za kurefusha maisha yao. Uongozi wako katika hili umekuwa imara na mzuri sana.”

Naye Mheshimiwa Sidibe amemwomba Rais Kikwete kuongoza kampeni ya kuhakikisha kuwa dawa za viwango vyote vya kupambana na ukimwi zinaanza kutengenezwa na kuzalishwa katika nchi zinazoendelea badala ya kutengenezwa katika nchi tajiri zinazoweka masharti makubwa katika kuruhusu dawa hizo kutengenezwa kwa bei rahisi zaidi katika nchi masikini.

“Mheshimiwa Rais tunakuomba uwe sauti yetu, tunakuomba uongoze msukumo mpya wa kutaka nchi masikini nazo ziwe na teknolojia ya kutengenezwa dawa bora zaidi za kukabiliana na ukimwi. Kama hatutaweza kuzizalisha dawa hizi kwenye nchi zetu itafikia mahali hata watu milioni tano wanapata dawa hizo katika Afrika wakajikuta hawapati dawa siku moja,” Mheshimiwa Sidibe amemwambia Rais Kikwete.

Monday, April 4, 2011

HOTUBA YA MWEZI KUTOKA KWA MKUU WA KAYA!!

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWA WANANCHI, TAREHE 31 MACHI, 2011
Ndugu Wananchi;
Kwa mara nyingine tena naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujaalia uhai na kutuwezesha kuwasiliana kwa utaratibu wetu wa kuzungumza kwa njia hii kila mwisho wa mwezi. Leo nina mambo matatu. La kwanza, linahusu shughuli niliyoifanya mwezi huu tunaoumaliza leo ya kutembelea Wizara na Idara za Serikali. Jambo la Pili ni kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Na jambo la tatu ni kuhusu mchakato wetu wa Katiba Mpya.

Ziara za Wizara
Ndugu Wananchi;

Kuanzia tarehe 15 Machi, 2011 nimekuwa nikifanya ziara ya kutembelea Wizara za Serikali na baadhi ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hizo. Madhumuni ya ziara hizo ni kufanya mambo matatu: Kwanza, kupata taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005 hadi 2010 na maagizo mbalimbali niliyotoa kwa Wizara miaka mitano iliyopita. Pili, ni kupata taarifa kuhusu jinsi Wizara zilivyojipanga kutekeleza majukumu yake na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010 – 2015. Na tatu, kutoa maelekezo maalum kwa mambo mbalimbali ninayotaka Wizara zifanye.

Ndugu Wananchi;
Mpaka sasa, nimekwishatembelea Wizara 14 na taasisi tatu za Serikali, yaani Mamlaka ya Mapato (Idara ya Forodha), Bandari ya Dar es Salaam na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Pia, nimeonana na kuzungumza na Mawakala wa Forodha. Kwa jumla ziara zangu zilikuwa nzuri na malengo niliyojiwekea yametimia. Nimefarijika sana kuona na kusikia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005 – 2010 na maagizo niliyoyatoa miaka mitano iliyopita. Aidha, nimeridhishwa na jinsi Wizara na Taasisi zao zilivyojipanga kutekeleza majukumu yao na Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015.

Ndugu Wananchi;
Pamoja na changamoto zilizojitokeza na zilizopo, malengo mengi sana tuliyojiwekea yametimia. Narudia kutoa pongezi za dhati kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika na inayoendelea kufanyika. Upo upungufu katika baadhi ya maeneo ambao unahitaji kusahihishwa. Sina shaka kabisa kuwa kwa mipango iliyopo na ari niliyoiona ya utekelezaji katika Wizara na taasisi nilizozitembelea kasoro hizo zitarekebishwa.

Mapato na Matumizi ya Serikali
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuzungumzia baadhi ya mambo niliyoyaona au kujitokeza katika ziara zangu hizo. Kwa kuanzia, naomba kuzungumzia suala la mapato na matumizi ya Serikali. Hali ya ukusanyaji wa mapato inaendelea vizuri hasa kuanzia Januari, 2011. Miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu wa fedha (Julai – Desemba, 2010) makusanyo ya mapato ya Serikali yalikuwa chini ya lengo kwa asilimia 8.

Makusanyo katika Idara ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ndiyo yaliyokuwa chini zaidi. Narudia kuwahimiza na kuwatia moyo ndugu zetu wa TRA na Hazina waendelee na kazi nzuri waifanyayo na kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyojitokeza. Niliambiwa kuwa moja ya sababu ya kuwepo matatizo kwa upande wa VAT ni mpango mpya unaowataka wafanyabiashara kutumia mashine maalum za kielektroniki za kutolea risiti na kuhifadhi kumbukumbu za mauzo (Electronic Fiscal Devices – EFD). Mashine hizo zinapotumika kodi ya Serikali hujulikana kwa uhakika hivyo ni rahisi kuifuatilia kwa wafanyabiashara. Kila risiti inapotolewa taarifa hupatikana TRA moja kwa moja, hivyo si rahisi kukwepa kodi. Mashine hizo bado hazijaenea kote na baadhi ya wafanyabiashara hawazipendi, ndiyo maana kuna matatizo kwenye makusanyo ya VAT.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa maombi matatu: Ombi la kwanza ni kwa wafanyabiashara. Nawaomba watoe ushirikiano kwa TRA kwa kutumia mashine hizo. Ni utaratibu utakaowaondolea usumbufu wanaoulalamikia wafanyabiashara kuhusu baadhi ya maofisa waonevu au wasiokuwa waaminifu na waadilifu. Kama kuna malalamiko yoyote kuhusu utekelezaji wa mpango huu, wawaone viongozi wa TRA au hata wa Wizara ya Fedha. Nawasihi viongozi wa TRA nao kutengeneza utaratibu mzuri wa kuwasikiliza wafanyabiashara ili yale matatizo yanayowakabili wayatatue. Aidha, waharakishe taratibu za upatikanaji wa mashine hizo na kutafuta njia za kuwasaidia wafanyabishara wadogo waweze kumudu kuzipata. Ningependa jambo hili lifanyike haraka ili utekelezaji wa mpango huu mzuri uende kwa kasi nzuri. Hilo ndilo ombi langu la pili.

Ndugu Wananchi;
Ombi la tatu ni kwa wananchi wenzangu kudai kupewa risiti kwa kila manunuzi wanayoyafanya dukani. Naomba mtambue kuwa kila unaponunua kitu dukani umeshalipa kodi. Hivyo basi unapoacha kudai risiti pesa ile ya kodi umemuachia mfanyabiashara na unainyima Serikali yako mapato ambayo ikiyapata yanaiongezea uwezo wa kuwahudumia wananchi wake pamoja na wewe.
Tafadhalini sana, msikubali kuwaacha wafanyabiashara wanufaike badala ya wananchi walio wengi. Nawaomba Watanzania wenzangu tukumbuke kuwa kulipa kodi au kusaidia kodi kulipwa ni wajibu wa msingi wa raia na ni kitendo cha uzalendo wa hali ya juu. Kufanya kinyume chake ni kukosa moyo wa uzalendo na kuvunja sheria. Raia mwema ni mlipa kodi mzuri na husaidia kuzuia watu wengine anaowajua au anaowaona wasikwepe kulipa kodi. Nawaomba sote: wafanyabiashara na raia tutimize ipasavyo wajibu wetu huo. “Inawezekana. Kila mtu atimize wajibu wake!”

Nidhamu ya Matumizi
Ndugu Wananchi;
Juhudi za kuongeza mapato ya Serikali zitakuwa na maana iwapo kutakuwa na matumizi mazuri ya fedha za Serikali. Jambo hili nimekuwa nalisisitiza mara kwa mara na nililirudia tena nilipozungumza na viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Niliwakumbusha wajibu wao wa kuhakikisha kuwa fedha na mali za umma zinatumiwa vizuri na kwamba sheria na kanuni za manunuzi ya umma zinazingatiwa katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma. Aidha, niliwakumbusha kuwa wasichelee kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali za umma na kukiuka sheria na kanuni za fedha na manunuzi ya umma.

Maslahi ya Watumishi
Ndugu Wananchi,
Nilipokuwa Wizara ya Utumishi, nilisisitiza suala zima la kuboresha utendaji wa watumishi wa umma nchini pamoja na umuhimu wa kuendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya watumishi hao. Aidha, niliwataka wahakikishe kuwa ucheleweshaji uliotokea safari hii kuhusu ajira ya walimu waliokwishahitimu mafunzo yao vyuoni haujirudii tena. Niliwaelekeza wakae mapema na wenzao wa Hazina, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kujua walimu wangapi wanatarajiwa kuhitimu katika mwaka husika wa fedha ili stahili zao na mishahara yao itengwe katika bajeti.

Niliagiza pia kwamba utaratibu huo utumike kwa madaktari na wauguzi ili mara wataalamu hao wanapohitimu masomo yao waweze kuajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi. Vile vile, nimewakumbusha umuhimu wa kuhakikisha kwamba watumishi wapya wanaoajiriwa wanalipwa mishahara na stahili zao mara wanapowasili katika vituo vyao na kuanza kazi. Watumishi kukaa miezi kadhaa bila ya kulipwa mishahara na stahili nyingine ni jambo linalosikitisha, halikubaliki na kwamba wakati umefika lisiendelee kutokea.

Ndugu Wananchi;
Pamoja na hayo nimesisitiza kuwa mtumishi kupandishwa cheo ni stahili yake na ni haki yake ya msingi. Hivyo, wakati wake unapofika na kama hakuna sababu za msingi, lazima apandishwe cheo. Pale mtumishi anaponyimwa kupandishwa cheo wakati wake ukifika, ni vyema aelezwe sababu ili ajirekebishe. Hii pia itampa fursa ya kukata rufaa kwa mamlaka za juu iwapo hakuridhika na sababu zilizotolewa. Nimekumbusha pia kwamba watumishi wanaopandishwa vyeo mishahara yao irekebishwe mapema iwezekanavyo. Nimewataka wawajibishe maafisa wakuu wasiotimiza wajibu wao ipasavyo na kusababisha ucheleweshaji na usumbufu usiokuwa wa lazima kwa watumishi wa umma. Kwa wale waliosababisha Serikali kupata hasara kwa kulipa watumishi hewa hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao bila ajizi.

Uwekezaji Katika Shule za Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa elimu, nilipata taarifa kuhusu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupanua fursa za vijana wetu kupata elimu, tangu ya awali mpaka elimu ya juu na mafunzo ya ufundi. Aidha, nimeelezwa hatua thabiti zinazochukuliwa za kuongeza ubora wa elimu ambazo pia zinajumuisha kuboresha maslahi na huduma kwa walimu na wakufunzi. Vile vile, nilielezwa changamoto zinazokabili sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na mikakati ya kukabiliana nazo. Nimewapongeza kwa juhudi hizo na kuwataka waendelee nazo, nami nimewaahidi msaada wangu bila ya kuchoka.

Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa changamoto ambayo nitapenda kuizungumzia ni ile ya mahitaji makubwa ya nafasi za kidato cha 5 na cha 6 kwa vijana wetu. Baada ya ujenzi wa sekondari nyingi za kata, kumeanza kujitokeza ongezeko kubwa la wanafunzi watakaomaliza kidato cha nne wanaohitaji kuendelea na masomo ya kidato cha tano. Idadi itaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka. Hivi sasa nafasi za kidato cha tano zilizopo Serikalini ni 37,300 na mipango inaendelea ya ujenzi wa shule zenye kidato cha tano na sita katika kila tarafa. Hata hivyo, nachelea kuwa bado hazitakidhi mahitaji makubwa yanayoongezeka kila mwaka. Jambo hili lisiachiwe Serikali peke yake.
Napenda kutumia nafasi hii kurudia ombi nililotoa Dodoma hivi karibuni kwa mashirika ya dini na watu binafsi wasaidiane na Serikali kubeba mzigo huu. Naomba wajenge shule zenye kidato cha 5 na 6. Wakati huo huo nawahimiza viongozi wa Serikali wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa lengo la kila tarafa kuwa na shule yenye kidato cha 5 na 6 linatekelezwa kwa ukamilifu.

Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Ndugu Wananchi;
Nilipotembelea Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, nimepata faraja kuwa utekelezaji wa malengo yetu ya kuleta mageuzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi yanakwenda vizuri. Nimefurahi kuona kwamba muelekeo wa miaka mitano ijayo ni mzuri. Nimeelezwa changamoto mbalimbali zinazozikabili sekta zetu hizi na nimefurahishwa na mikakati ya Wizara zetu mbili ya kukabiliana nazo. Nilifarijika sana kusikia kuwa mipango kabambe ya kuendeleza ufugaji na uvuvi imekamilika. Mimi nimewaahidi kuwasemea kwa wanaotoa mgao wa fedha ili wawezeshwe kutekeleza malengo yao.

Ndugu Wananchi;
Hizi ni sekta muhimu sana, hivyo kuendelezwa kwake kunawanufaisha Watanzania wengi. Ukizungumzia kupunguza na hatimaye kuondoa umaskini nchini huwezi kufanikiwa bila kuendeleza sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi ambazo asilimia 80 ya Watanzania huzitegemea.

Nilipozitembelea Wizara hizo nilisisitiza mambo manne ambayo ningependa muyafahamu. Jambo la kwanza linahusu kuutazama upya mfumo wa vocha za pembejeo ili kuleta ufanisi zaidi. Serikali imeanzisha mpango wa kutoa ruzuku kwa pembejeo za kilimo kama vile mbegu, mbolea na dawa. Mpango huu una nia ya kuwaongezea wakulima uwezo wa kupata mavuno zaidi ili waongeze kipato chao na kuinua hali zao za maisha. Tulianzisha mfumo wa vocha ili kuhakikisha kuwa ruzuku hiyo inawafikia wahusika. Kuanzia miaka miwili iliyopita kumejitokeza vitendo viovu vinavyofanywa na wajanja wachache ambavyo ni kinyume na matazamio ya Serikali. Nilishaagiza vyombo vya dola kuwasaka wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria. Kazi hiyo inaendelea ingawaje naomba kasi na nguvu iongezeke.

Pamoja na kufanya hayo, nimeagiza tuuangalie upya mfumo wetu wa ugawaji wa pembejeo za ruzuku. Kama kuna upungufu wowote tuurekebishe, tuzibe mianya inayotumiwa na wahalifu ili ufanisi zaidi upatikane. Nimefurahishwa na taarifa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameanza kuufanyia ukaguzi mfumo wa ugawaji pembejeo ili atoe mapendekezo ya namna ya kuuboresha. Vile vile, nimefurahishwa na uamuzi wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wa kupeleka watu Malawi ili wakajifunze kutokana na uzoefu wa wenzetu.

Jambo la pili, linahusu kuanzisha mfumo wa masoko ya mazao ili wakulima wawe na masoko ya uhakika na yanayotoa bei nzuri. Ni jambo ambalo nimekuwa nalihimiza tangu niingie madarakani. Nilifurahi sana nilipoambiwa kuwa hivi sasa mchakato wa kuanzisha “Soko la Mazao ya Kilimo” yaani Commodity Exchange Market uko mbioni kuanza. Narudia kuwapongeza sana na kuwatakia mafanikio mema na ninawaahidi msaada wangu pale itakapostahili.

Jambo la tatu, ni kwamba nimezielekeza Wizara zinazohusika na kilimo na mifugo kushirikiana na TAMISEMI kuanza kupeleka wahitimu wa vyuo vikuu katika ngazi ya tarafa na kata ili wasaidie kuinua ubora wa kilimo na ufugaji miongoni mwa wananchi. Na, jambo la nne ninalopenda kulisemea, ni kutoa pongezi kwa Idara ya Uvuvi kwa kazi kubwa waifanyayo ya kupambana na uvuvi usiokuwa endelevu pamoja na uvuvi haramu. Narudia kuwahakikishia utayari wangu na wa Serikali kuwasaidia kuwajengea uwezo wa kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Hifadhi ya Taifa
Ndugu Wananchi;
Nimetembelea Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula kukagua na kupata taarifa ya shughuli zao. Nimefarijika sana kusikia kuwa malengo tuliyowawekea ya kuhifadhi tani 200,000 za mahindi mwaka huu wameyafikia na kwamba sasa wana akiba ya tani 217,000 katika maghala yao. Nimefurahishwa sana na taarifa ya jinsi Wakala hiyo inavyojiandaa kutekeleza agizo langu la kupanua uwezo wa hifadhi yetu hadi kufikia tani 400,000 mwaka 2015.

Ndugu Wananchi;
Jambo jipya ambalo nimeagiza Hifadhi ifanye kuanzia sasa ni kushiriki katika kupunguza ukali wa bei za vyakula mijini, pindi kunapojitokeza upungufu wa chakula. Natambua kuwa kila kunapotokea upungufu wa chakula vijijini, Hifadhi ya Taifa imetumika kukabiliana na tatizo hilo. Nimewataka sasa wafanye hivyo kwa mijini, kwa kuwauzia mahindi wafanyabiashara katika masoko yanayouza vyakula pale unapotokea upungufu wa mahindi yanayoletwa katika masoko.

Wakifanya hivyo, bei za mahindi zitashuka na hivyo kupunguza mfumuko wa bei kwa upande wa chakula.
Nimezungumzia mahindi kwa sababu kwa sasa hifadhi yetu hununua mahindi na mtama tu. Nimewaagiza kuwa, kwa siku za usoni waanze kuangalia uwezekano wa kununua kiasi fulani cha mchele na kuuhifadhi kwa nia ya kuuza baadae ili kupunguza makali ya bei ya chakula hicho pale, kunapotokea upungufu.

Uchukuzi
Ndugu wananchi;
Kwa upande wa Wizara ya Uchukuzi, nimerudia maelekezo yangu ya kawahimiza kuharakisha mchakato wa Shirika letu la reli kuachana na RITES na mchakato wa kuboresha reli ya Kati na TAZARA. Nimefurahi kusikia kwamba mchakato wa kununua meli mpya katika Maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Niliarifiwa kuwa tayari wataalam washauri kutoka Denmark wamekwishaanza kufanya upembuzi yakinifu juu ya aina ya meli itakayofaa katika Ziwa Victoria. Nimewaagiza, waharakishe kukamilisha mchakato huo ili waendelee na zoezi kama hilo katika Maziwa Nyasa na Tanganyika na hatimaye ununuzi wa Meli ufanyike.

Hali ya Umeme Nchini
Ndugu Wananchi;
Mgao wa umeme bado unaendelea nchini, ingawaje kwa muda wa wiki moja hivi kumekuwepo na nafuu kidogo. Hii imetokana na maji kuongezeka katika mabwawa ya Kihansi na Kidatu kutokana na mvua zinazonyesha katika milima ya Udzungwa. Kwa sababu hiyo, uzalishaji wa umeme katika mabwawa hayo umeongezeka kiasi na kuleta nafuu kidogo iliyopo sasa.

Hata hivyo, ahueni hii si ya kutegemea sana kwani hali katika bwawa la Mtera bado siyo nzuri, hivyo siku yoyote mvua hizo zitakaposimama au kupungua katika milima ya Udzungwa mgao utarudi kwa makali yake ya awali. Hadi leo nizungumzapo nanyi, kina cha maji katika bwawa la Mtera kimefikia mita 690.88 ambacho bado ni chini sana. Maji yapo juu ya kina cha ukomo wa chini kwa sentimeta 88 tu, hivyo bado tuna safari ndefu mpaka kufikia kina cha juu cha mita 698. Tuzidi kumuomba Mola mvua kubwa zinyeshe katika milima na mabonde ya mito inayoingiza maji katika Bwawa la Mtera.

Ndugu Wananchi;
Kama nilivyokwishaeleza, hivi sasa TANESCO wanaendelea na mchakato wa ukodishaji wa mitambo ya dharura ya kufua umeme wa megawati 260. Tayari zabuni imekwishatangazwa ili kumpata mkandarasi atakayekidhi viwango na mwenye gharama nafuu. TANESCO wameahidi kuwa ifikapo mwezi Julai uzalishaji wa umeme huo wa dharura utakuwa umeanza. Nimewaagiza TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha kuwa mpango huo unatekelezwa kama ilivyopangwa. Aidha, nimewataka waongeze kasi ya kutekeleza mipango mingine ya kulipatia taifa umeme wa uhakika na endelevu katika kipindi kifupi kijacho.

Gharama za Kuunganisha Umeme
Ndugu Wananchi;
Jambo jingine ambalo niliwataka TANESCO waliangalie haraka ni lile la gharama kubwa za kuwaunganishia wateja umeme. Gharama hizo zinawakwaza wananchi wengi kupata umeme. Nimewataka waangalie uwezekano wa kuzipunguza au hata kuwaunganishia watu umeme na kuingiza gharama hizo katika bili za umeme za kila mwezi. Nimewasihi kuwa iwapo wataamua hivyo, wawape muda wa kutosha wa kulipa. Usiwe muda mfupi kwani utakuwa mzigo mkubwa mno kwao. Nimewakumbusha pia kuwa tunalo lengo la kuwapatia umeme asilimia 30 ya Watanzania ifikapo 2015. Lengo hilo halitafanikiwa iwapo hatutatafuta namna ya kupunguza gharama au kutoa nafuu katika kuunganisha umeme kwa watu.

Matukio ya Ujangili katika Hifadhi
Ndugu Wananchi;
Nilipotembelea Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na mambo mengine, tulizungumzia tatizo la kuongezeka kwa vitendo vya ujangili katika mbuga za wanyama zinazoangaliwa na Serikali au mashirika yake. Kuna kila dalili kwamba mamlaka za hifadhi zetu zinaelekea kuelemewa na majangili. Nimewaagiza waongeze juhudi na nimewaambia kuwa niko tayari kuagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kusaidia kupambana na majangili. Nchi yetu inayo historia ya kufanya hivyo mwaka 1989 kwa mafanikio. Niko tayari kufanya hivyo tena.

Jambo lingine ambalo nililizungumzia ni mchakato wa Wizara wa kutaka kuitangaza misitu ya milima ya Tao la Mashariki yaani milima ya Pare, Usambaa, Uluguru, Nguu hadi misitu ya Udzungwa kuwa urithi wa dunia (World Heritage Site). Lengo linaweza kuwa zuri kwamba nchi yetu inaweza kupata misaada ya kuhifadhi misitu hiyo. Lakini, uamuzi huo una maana kubwa kwa watu wa maeneo hayo, mamlaka za Serikali za Mitaa na hata nchi kwa jumla. Kwa mujibu wa utaratibu uliopo, watu au hata mamlaka ya nchi haitaweza kuamua kufanya jambo lolote katika maeneo hayo bila ya kupata kibali cha UNESCO.

Ndugu Wananchi;
Kwa Tanzania kufanya kitu cha namna hiyo si jambo la ajabu kwani tunayo maeneo kadhaa ambayo tumekwishayaingiza kwenye kundi la urithi wa dunia. Hata hivyo, inatakiwa pawepo na mashauriano mapana na wadau wote na kuafikiana kabla ya kupeleka maombi UNESCO. Bahati mbaya kwa suala hili haikufanyika hivyo, jambo ambalo siyo sawa. Niliwataka waondoe maombi hayo na kama wanaona ifanyike hivyo, tupate muda wa kutosha wa kushauriana na kukubaliana ipasavyo.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali
Ndugu Wananchi;
Tarehe 29 Machi 2011 Ndugu Ludovick Utouh, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alinikabidhi Ripoti za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma kwa mwaka 2009/2010. Amefanya hivyo kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ibara ya 143 (iv). Nami kwa mujibu wa matakwa ya Katiba hiyo, nimeshawasilisha taarifa hizo kwa Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha kwa ajili ya kuziwasilisha Bungeni.

Narudia tena kumshukuru sana Ndugu Ludovick Utouh na wakaguzi wenzake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kukagua hesabu za Serikali. Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zimekuwa kioo kizuri kwetu sisi katika Serikali kujiona na kujipima jinsi tunavyotimiza wajibu wetu kuhusu sheria na kanuni za fedha na manunuzi ya umma.

Ndugu Wananchi;
Inatia moyo kuona kuwa, idadi kubwa ya Wizara na Halmashauri zinaendelea kufanya vizuri na kupata hati zinazoridhisha. Hata hivyo, haifurahishi kuona kuwa idadi hiyo imepungua kuliko ile ya mwaka 2008/2009. Inasikitisha pia kwamba idadi ya Halmashauri za wilaya zilizopata hati chafu imeongezeka kutoka moja mwaka 2008/2009 na kuwa nne mwaka 2009/10. Kwa upande wa Serikali Kuu hapakuwepo na mabadiliko kwani idadi ya hati zisizoridhisha imebaki ile ile, yaani Mkoa mmoja na Idara moja kama ilivyokuwa mwaka uliopita. Lakini, baya zaidi ni mkoa huo huo na hali ya hesabu za Halmashauri nchini bado zina mapungufu mengi hivyo kuhitaji hatua maalum kuchukuliwa ili kuondokana na aibu hiyo.

Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia maagizo niliyoyatoa miaka ya nyuma ya kutaka viongozi na watendaji wakuu wa kila Wizara, Taasisi ya Serikali na Mashirika ya Umma yaliyokaguliwa kuisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu maeneo yao. Kisha wachukue hatua zipasazo kusahihisha kasoro zilizojitokeza katika maeneo yao ya uongozi na utendaji. Kwa makosa yanayojirudia mwaka hadi mwaka na yale ya wizi na ubadhilifu, mamlaka ya juu kwa kila ngazi ichukue hatua stahiki za kinidhamu na kisheria kwa wahusika.

Nampongeza sana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kwa kuanza na kuendelea na ukaguzi wa ufanisi katika baadhi ya taasisi za Serikali. Nafurahi pia kwamba ameahidi kufanya kwa upana zaidi ukaguzi wa thamani ya fedha zaidi ya ukaguzi wa hesabu. Sote tuwatakie mafanikio mema ili fedha na rasilimali kidogo tulizonazo zifanye kazi iliyokusudiwa na kunufaisha walengwa.

Mchakato wa Katiba
Ndugu Wananchi;
Katika Hotuba yangu ya Mwisho wa Mwaka, niliahidi kwamba tutaanzisha mchakato wa kuhuisha Katiba ya nchi yetu. Tayari tumeanza utekelezaji wa ahadi hiyo. Katika kikao cha Bunge kitakachoanza Jumanne, wiki ijayo, muswada wa sheria kwa ajili ya kusimamia mchakato huo utawasilishwa na Serikali. Miongoni mwa mambo mengine, Muswada huo umeainisha utaratibu wa uundwaji wa Tume ya Katiba (Constitutional Review Commission), utaratibu wa kukusanya maoni, uundwaji wa Bunge la Katiba na wananchi kupiga kura ya maoni kupitisha Katiba hiyo (referendum).
Utaratibu unaopendekezwa umejengeka juu ya msingi wa kuwahusisha wananchi wote wanaostahili kushiriki katika mchakato wa uundwaji wa Katiba yao mpya. Mchakato huu ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu, hivyo kila mmoja wetu ajitahidi kushiriki kutoa maoni yake kadri anavyoona inafaa wakati ukifika.

Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Naomba nimalizie kwa kuwashukuru wananchi kwa kuendelea kuiunga mkono na kuisaidia Serikali yenu. Tuendelee kufanya kazi kwa bidii na maarifa kwa maslahi ya kila mmoja wetu, familia zetu na nchi yetu kwa ujumla.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!