Tuesday, March 15, 2011

ZIARA YA RAIS KIKWETE HAZINA YAIBUA MAMBO MENGI!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Jumanne, Machi 15, 2011, ametembelea Wizara ya Fedha (Hazina), ikiwa ni mwanzo wa ziara za kutembelea Wizara mbalimbali kujionea utendaji wa Serikali, kuangalia utekelezaji wa maagizo ya Serikali na yale aliyoyatoa alipotembelea wizara zote mwanzoni mwa mwaka 2006, mwezi mmoja tu baada ya kuwa ameingia madarakani.

Aidha, Rais baada ya kuwa ametembelea Wizara ya Fedha ametembelea Kitengo cha Long Room cha Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA).

Katika mazungumzo na viongozi wa Wizara na taasisi zote zilizoko chini ya Wizara hiyo, Rais Kikwete ameelezea majukumu matatu makuu ya Wizara hiyo kama ifuatavyo:

(a) Kusimamia Kukua kwa Uchumi

Rais Kikwete amesema kuwa wajibu kipaumbele katika miaka mitano ijayo iwe ni kwa Wizara ya Fedha kusimamia na kutafuta njia za kuleta utulivu zaidi katika uchumi kwa kubuni mikakati bora zaidi ya kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi zaidi na hivyo kupunguza umasikini kwa haraka zaidi. Hivyo, Rais amesema kuwa hata Bajeti ya Serikali ni lazima ilenge katika sekta zitakazoharakisha zaidi kasi ya kukua kwa uchumi.

Sambamba na agizo hilo, Rais Kikwete pia ameielekeza Wizara ya Fedha kutafuta njia za haraka na bora zaidi za kupunguza mfumuko wa bei ili kuwapatia wananchi unafuu zaidi wa maisha.

(b) Ukusanyaji Mapato ya Serikali

Rais Kikwete amesisitiza kuwa Hazina ndiyo moyo na roho ya Serikali na kwamba Wizara hiyo isipofanya kazi ya kukusanya mapato ni dhahiri shughuli za Serikali zitaathirika.

Rais amewasifu watumishi wa Wizara ya Fedha kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali lakini akawataka waongeze juhudi zaidi na wafanye vizuri zaidi. Ameambiwa kuwa mapato ya Serikali yameongezeka kutoka makusanyo ya kiasi cha shilingi bilioni 215 kwa mwezi mwaka 2005 wakati Rais kikwete anaingia maradakani hadi kufikia wastani wa shilingi bilioni 420 kwa mwezi kwa sasa.

(C) Kusimamia Matumizi ya Fedha ya Serikali

Rais Kikwete amesema kuwa jukumu la tatu la msingi la Wizara hiyo ni kusimamia matumizi ya fedha zinazokusanywa akiwakumbusha viongozi hao kuwa fedha za Serikali siyo shamba la bibi na wala makusanyo hayo ya kodi siyo sawa na ubani wa kilioni.

Amesema kuwa fedha za Serikali baada ya kukusanywa ni lazima zitumike vizuri na kwa shabaha zilizokukusudiwa na akaelezea ni sababu hiyo iliyopelekea Serikali kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi wa matumizi ikiwa ni pamoja na kuunda nafasi ya Naibu Mhasibu Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kusimamia fedha zinazopelekwa kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na pia kuanzisha nafasi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali.

(D) Maagizo Mengine Makubwa

(i) Rais Kikwete amesema kuwa moja ya maeneo ambayo bado yana matatizo katika Wizara hiyo ni shughuli ya Manunuzi na ameitaka Wizara ya Fedha kuhakikisha kuwa wanaajiriwa watu wenye ujuzi na elimu ya masuala ya ununuzi lakini ambao pia ni waaminifu.

(ii) Rais Kikwete pia ameitaka Wizara hiyo kukabiliana na tatizo la kucheleweshwa kulipwa kwa mishahara mipya hasa ile ya watumishi wapya katika Serikali. Aidha, amerudia maelekezo yake kuwa Halmashauri nchini haziwezi kuruhusiwa kuhamishahamisha watumishi bila na kuwa na fedha za kulipia uhamisho huo.

(iii) Kuhusu malipo ya mishahara na marupurupu mengine ya watumishi, Rais Kikwete ametaka umakini mkubwa katika kuhakikisha kuwa haki za watumishi zinalindwa na watu hao kulipwa malipo yao ya haki na kwa wakati.

(iv) Kuhusu malipo ya wasataafu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika, Rais Kikwete ametaka wote wanaostahili kulipwa mafao yao na hawajalipwa hadi sasa walipwe, hata kama ni kweli kuwa wengi wa watumishi hao tayari wamelipwa.

(v) Kuhusu mikopo kwa watumishi wa Serikali, Rais Kikwete amesema amefurahishwa na kwamba Wizara ya Fedha inakamilisha taratibu za kuwakopesha watumishi hao, kama wanavyokopeshwa Wabunge. Aidha, ameongeza kuwa Wizara iangalie uwezekano wa hata kuwadhamini watumishi hao ili waweze kukopa moja kwa moja kwenye taasisi za fedha nchini.

(vi) Kuhusu Deni la Taifa, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la heri sana kuwa Tanzania sasa inakopesheka tena, lakini lazima Wizara ya Fedha itumie uangalifu mkubwa katika kukopa ili Tanzania ijikute inarudi tena katika mazingira yaliyopelekea kuachwa kukopeshwa huko nyuma.

No comments:

Post a Comment