Wednesday, March 23, 2011

CUF NAO WATUMA SALAMU ZAO ZA RAMBIRAMBI!!

Jumuiya ya Vijana ya CUF – (JUVICUF) tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya waimbaji wa Bendi ya Taarab (Five Stars Modern Taarab) vilivyotokea kwa ajali ya gari huko Mikumi Mkoani Morogoro wakati wakitokea Mbeya kuwapa Burudani wakazi wa huko.

Ajali za barabarani zimekuwa zikipoteza mamia ya roho za watanzania ambao wengi wao ni vijana jambo linalo sababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa letu, na nyingi ajali hizo zinatokana na uzembe wa madereva .

Jumuiya ya Vijana ya CUF – tunasisitiza serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Miundo Mbinu kutowafumbia macho madereva wazembe na kuhakikisha wanachukuliwa hatua kali za kisheria

Jumuiya ya Vijana ya CUF – tunaungana na watanzania wote kuwapa pole na kuwafariji ndugu, wapenzi wa muziki wa taarabu nchini pamoja na jamaa wa marehemu. tunawaomba kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo na tunamuomba mungu azilaze mahali pema peponi roho za marehemu hao.

Halikadhalika tunawaomba wale wote waliojeruhiwa wawe na subira na tunawaombea kwa mwenyezi mungu wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa letu.

No comments:

Post a Comment