Wednesday, March 9, 2011

RAIS KIKWETE SAFARINI ADDIS ABABA!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Machi 9, 2011, anaungana na marais wenzake wa Afrika waliopewa jukumu la kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Afrika Magharibi ya Ivory Coast, katika hatua za mwisho za jitihada za kujaribu kumaliza mgogoro huo.

Rais Kikwete na marais wenzake wanakutana mjini Addis Ababa, Ethiopia, katika jitihada mpya za kutafuta jawabu la mzozo huo uliolipuka mwishoni mwa mwaka jana kufuatia matokeo ya raundi ya pili ya uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo uliofanyika Novemba 28, 2011.

Katika mkutano huo wa siku mbili, marais hao wanatarajiwa kukabidhi ripoti yao kwa Kamati ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika (AU), ili kuuwezesha Umoja huo kuchukua uamuzi kamili wa jinsi ya kumaliza mgogoro huo.

Ripoti hiyo ni matokeo ya mikutano ya marais hao mjini Addis Ababa, huko Mauritania ambako walikutana mara mbili, na mjini Abidjan, Ivory Coast. Marais hao waliteuliwa na Kikao cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU katika mkutano wao wa Januari mwaka huu.

Rais Kikwete ameondoka nchini leo asubuhi kwenda Ethiopia kwa kikao hicho cha siku mbili ambako ataungana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Idriss Deby wa Chad, Rais Blaise Campaore wa Burkina Faso na Rais Mohamed Abdel Aziz ambaye ni mwenyekiti wa kundi hilo.

Wengine wanaotarajiwa kushiriki katika kikao hicho ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Bwana Jean Ping na wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Mataifa (UN).

Mzozo wa Ivory Coast ulianza baada ya taasisi mbili zinazosimamia uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo tofauti ya washindi wa raundi hiyo ya pili ya upigaji kura kati ya Mheshimiwa Laurent Gbagbo, aliyekuwa anatetea kiti chake na mpinzani wake mkuu, Mheshimiwa Alassane Quattara.

Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Quattara kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia tisa, lakini siku nne baadaye, Baraza la Katiba la nchi hiyo lilimtangaza Gbagbo kuwa mshindi kwa asilimia moja.

Baraza hilo lilimtangaza Gbagbo mshindi baada ya kuwa limefuta matokeo katika majimbo saba aliyokuwa ameshinda Quattara, kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiko ngome kuu yake ya kisiasa. Kwa kufuta matokeo katika majimbo hayo, Baraza lilimpunguzia Quattara kura 600,000.

Tokea wakati huo, viongozi hao wawili wote wamejitangaza marais na kila mmoja kuunda Serikali yake. Nchi hiyo sasa imetumbukia katika mgogoro kamili wa kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambako yamekuwepo mauaji ya watu na uharibifu mkubwa wa mali nchini humo.

No comments:

Post a Comment