Wednesday, March 23, 2011

IKULU YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA WASANII WA FIVE STARS!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi kutokana na vifo vya wasanii 13 wa Kundi la Muziki wa Taarab la Five Star Modern Taarab.

Wasanii hao waliokuwa kwenye gari la kukodi wakitokea Kyela, Mbeya, walipata ajali eneo la Doma, karibu na Mbuga ya Wanyama ya Mikumi, Mkoani Mororogoro usiku wa kuamkia tarehe 22 Machi, 2011 wakati gari hilo lilipogongana na gari lingine. Wasanii hao walikuwa wakirejea Dar es Salaam kutoka Mbeya ambako walikuwa wamefanya maonyesho.

Watu 12 walifariki hapo hapo, mwingine akafariki njiani akikimbizwa hospitali na watu wengine wanane kujeruhiwa kwa viwango tofauti.

“Binafsi nimeguswa mno na msiba huu kwa vile umetupotezea wasanii ambao walikuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza sanaa ya muziki wa Taarab nchini kwetu. Hili ni pigo kubwa siyo kwa usanii wa Taarab bali kwa Taifa letu zima la Tanzania.” Amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Ameongeza Mheshimiwa Rais katika salamu zake: “Nakutaka Mheshimiwa Waziri kupitia kwako ufikishe salamu zangu hizi za rambirambi kwa ndugu wa wafiwa wote. Wajulishe kuwa moyo wangu uko nao katika wakati huu mgumu na kuwa msiba wao ni msiba wetu sote.”

Rais Kikwete amesema anamwomba Mwenyezi Mungu azilaze mahali pema peponi roho za Marehemu wote huku akiwaomba waliopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo mbaya kuwa na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Vilevile Rais Kikwete anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo mbaya wapone haraka ili waweze kurejea katika hali yao ya kawaida na kuungana tena na familia, ndugu, jamaa na marafiki zao.

No comments:

Post a Comment