Wednesday, March 23, 2011

CUF NAO WATUMA SALAMU ZAO ZA RAMBIRAMBI!!

Jumuiya ya Vijana ya CUF – (JUVICUF) tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya waimbaji wa Bendi ya Taarab (Five Stars Modern Taarab) vilivyotokea kwa ajali ya gari huko Mikumi Mkoani Morogoro wakati wakitokea Mbeya kuwapa Burudani wakazi wa huko.

Ajali za barabarani zimekuwa zikipoteza mamia ya roho za watanzania ambao wengi wao ni vijana jambo linalo sababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa letu, na nyingi ajali hizo zinatokana na uzembe wa madereva .

Jumuiya ya Vijana ya CUF – tunasisitiza serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Miundo Mbinu kutowafumbia macho madereva wazembe na kuhakikisha wanachukuliwa hatua kali za kisheria

Jumuiya ya Vijana ya CUF – tunaungana na watanzania wote kuwapa pole na kuwafariji ndugu, wapenzi wa muziki wa taarabu nchini pamoja na jamaa wa marehemu. tunawaomba kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo na tunamuomba mungu azilaze mahali pema peponi roho za marehemu hao.

Halikadhalika tunawaomba wale wote waliojeruhiwa wawe na subira na tunawaombea kwa mwenyezi mungu wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa letu.

IKULU YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA WASANII WA FIVE STARS!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi kutokana na vifo vya wasanii 13 wa Kundi la Muziki wa Taarab la Five Star Modern Taarab.

Wasanii hao waliokuwa kwenye gari la kukodi wakitokea Kyela, Mbeya, walipata ajali eneo la Doma, karibu na Mbuga ya Wanyama ya Mikumi, Mkoani Mororogoro usiku wa kuamkia tarehe 22 Machi, 2011 wakati gari hilo lilipogongana na gari lingine. Wasanii hao walikuwa wakirejea Dar es Salaam kutoka Mbeya ambako walikuwa wamefanya maonyesho.

Watu 12 walifariki hapo hapo, mwingine akafariki njiani akikimbizwa hospitali na watu wengine wanane kujeruhiwa kwa viwango tofauti.

“Binafsi nimeguswa mno na msiba huu kwa vile umetupotezea wasanii ambao walikuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza sanaa ya muziki wa Taarab nchini kwetu. Hili ni pigo kubwa siyo kwa usanii wa Taarab bali kwa Taifa letu zima la Tanzania.” Amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Ameongeza Mheshimiwa Rais katika salamu zake: “Nakutaka Mheshimiwa Waziri kupitia kwako ufikishe salamu zangu hizi za rambirambi kwa ndugu wa wafiwa wote. Wajulishe kuwa moyo wangu uko nao katika wakati huu mgumu na kuwa msiba wao ni msiba wetu sote.”

Rais Kikwete amesema anamwomba Mwenyezi Mungu azilaze mahali pema peponi roho za Marehemu wote huku akiwaomba waliopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo mbaya kuwa na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Vilevile Rais Kikwete anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo mbaya wapone haraka ili waweze kurejea katika hali yao ya kawaida na kuungana tena na familia, ndugu, jamaa na marafiki zao.

Wednesday, March 16, 2011

MOURINHO AVUNJA MWIKO KWA LYON!!



Klabu ya Real Madrid imefanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainal baada ya kuvunja mwiko wa kuwa kibondr mbele ya Olympique Lyon baada ya kushinda kwa magoli 3-0. Klabu ya Chelsea nayo imesonga mbele baada ya kutoka sare ya 0-0 dhidi ya FC Copenhagen!!

CUF WAANZA KUWASHUKURU WAPIGA KURA!!

Waheshimiwa waandishi wa Habari, CUF- Chama Cha Wananchi kitafanya ziara ya awali ya kuwashukuru wapigakura katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, kisiwa cha Unguja, Lindi, Mtwara na Pwani kuanzia tarehe 19/03/2011 hadi tarehe 02/04/2011.

Ziara itaongozwa na Mwenyekiti wa CUF - Taifa, Prof. Ibrahimu Haruna Lipumba akifuatana na Kaimu Naibu Katibu Mkuu - Bara, Mhe. Julius Mtatiro, Wajumbe wa Baraza kuu la Uongozi - Taifa, Kiongozi wa wabunge wanaotokana na CUF ( Mh. Hamad Rashidi) na baadhi ya wabunge wanaotokana na CUF.



Malengo

· Kuwashukuru wabiga kura kwa kukipigia Chama Cha Wananchi (CUF) katika uchaguzi mkuu wa 31, Oktoba, 2010

· Kuishitaki kwa wananchi serikali ya CCM kwa kushindwa kuboresha maisha ya wananchi wake na kusababisha:-

o Kukosekana kwa umeme wa uhakika,

o Kupanda kwa gharama za maisha mfano bidhaa, nauli, na nk,

o Matatizo makubwa katika sekta ya afya,

o Uhaba wa maji , ukosefu wa ajira

o Miundombinu mibovu ya barabara, reli na nk

o Matatizo katika sekta ya Elimu na pia:-

Kuitaka Serikali ya CCM kuhakikisha kuwa mchakato wa Tume Huru ya Uchaguzi unafanyika mapema bila kusubiri mchakato wa kupata Katiba Mpya ya nchi.

CUF- Chama Cha Wananchi tunaamini kuwa ziara hii ni muhimu kwa wananchi wote,na tutatumia fursa hii kuwahakikishia wananchi kwamba CUF iko bega kwa bega na wananchi wote bila kujali itikadi zao za rangi, dini au kabila ili kuwaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi na kijamii.

Tuesday, March 15, 2011

ZIARA YA RAIS KIKWETE HAZINA YAIBUA MAMBO MENGI!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Jumanne, Machi 15, 2011, ametembelea Wizara ya Fedha (Hazina), ikiwa ni mwanzo wa ziara za kutembelea Wizara mbalimbali kujionea utendaji wa Serikali, kuangalia utekelezaji wa maagizo ya Serikali na yale aliyoyatoa alipotembelea wizara zote mwanzoni mwa mwaka 2006, mwezi mmoja tu baada ya kuwa ameingia madarakani.

Aidha, Rais baada ya kuwa ametembelea Wizara ya Fedha ametembelea Kitengo cha Long Room cha Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA).

Katika mazungumzo na viongozi wa Wizara na taasisi zote zilizoko chini ya Wizara hiyo, Rais Kikwete ameelezea majukumu matatu makuu ya Wizara hiyo kama ifuatavyo:

(a) Kusimamia Kukua kwa Uchumi

Rais Kikwete amesema kuwa wajibu kipaumbele katika miaka mitano ijayo iwe ni kwa Wizara ya Fedha kusimamia na kutafuta njia za kuleta utulivu zaidi katika uchumi kwa kubuni mikakati bora zaidi ya kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi zaidi na hivyo kupunguza umasikini kwa haraka zaidi. Hivyo, Rais amesema kuwa hata Bajeti ya Serikali ni lazima ilenge katika sekta zitakazoharakisha zaidi kasi ya kukua kwa uchumi.

Sambamba na agizo hilo, Rais Kikwete pia ameielekeza Wizara ya Fedha kutafuta njia za haraka na bora zaidi za kupunguza mfumuko wa bei ili kuwapatia wananchi unafuu zaidi wa maisha.

(b) Ukusanyaji Mapato ya Serikali

Rais Kikwete amesisitiza kuwa Hazina ndiyo moyo na roho ya Serikali na kwamba Wizara hiyo isipofanya kazi ya kukusanya mapato ni dhahiri shughuli za Serikali zitaathirika.

Rais amewasifu watumishi wa Wizara ya Fedha kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali lakini akawataka waongeze juhudi zaidi na wafanye vizuri zaidi. Ameambiwa kuwa mapato ya Serikali yameongezeka kutoka makusanyo ya kiasi cha shilingi bilioni 215 kwa mwezi mwaka 2005 wakati Rais kikwete anaingia maradakani hadi kufikia wastani wa shilingi bilioni 420 kwa mwezi kwa sasa.

(C) Kusimamia Matumizi ya Fedha ya Serikali

Rais Kikwete amesema kuwa jukumu la tatu la msingi la Wizara hiyo ni kusimamia matumizi ya fedha zinazokusanywa akiwakumbusha viongozi hao kuwa fedha za Serikali siyo shamba la bibi na wala makusanyo hayo ya kodi siyo sawa na ubani wa kilioni.

Amesema kuwa fedha za Serikali baada ya kukusanywa ni lazima zitumike vizuri na kwa shabaha zilizokukusudiwa na akaelezea ni sababu hiyo iliyopelekea Serikali kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi wa matumizi ikiwa ni pamoja na kuunda nafasi ya Naibu Mhasibu Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kusimamia fedha zinazopelekwa kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na pia kuanzisha nafasi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali.

(D) Maagizo Mengine Makubwa

(i) Rais Kikwete amesema kuwa moja ya maeneo ambayo bado yana matatizo katika Wizara hiyo ni shughuli ya Manunuzi na ameitaka Wizara ya Fedha kuhakikisha kuwa wanaajiriwa watu wenye ujuzi na elimu ya masuala ya ununuzi lakini ambao pia ni waaminifu.

(ii) Rais Kikwete pia ameitaka Wizara hiyo kukabiliana na tatizo la kucheleweshwa kulipwa kwa mishahara mipya hasa ile ya watumishi wapya katika Serikali. Aidha, amerudia maelekezo yake kuwa Halmashauri nchini haziwezi kuruhusiwa kuhamishahamisha watumishi bila na kuwa na fedha za kulipia uhamisho huo.

(iii) Kuhusu malipo ya mishahara na marupurupu mengine ya watumishi, Rais Kikwete ametaka umakini mkubwa katika kuhakikisha kuwa haki za watumishi zinalindwa na watu hao kulipwa malipo yao ya haki na kwa wakati.

(iv) Kuhusu malipo ya wasataafu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika, Rais Kikwete ametaka wote wanaostahili kulipwa mafao yao na hawajalipwa hadi sasa walipwe, hata kama ni kweli kuwa wengi wa watumishi hao tayari wamelipwa.

(v) Kuhusu mikopo kwa watumishi wa Serikali, Rais Kikwete amesema amefurahishwa na kwamba Wizara ya Fedha inakamilisha taratibu za kuwakopesha watumishi hao, kama wanavyokopeshwa Wabunge. Aidha, ameongeza kuwa Wizara iangalie uwezekano wa hata kuwadhamini watumishi hao ili waweze kukopa moja kwa moja kwenye taasisi za fedha nchini.

(vi) Kuhusu Deni la Taifa, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la heri sana kuwa Tanzania sasa inakopesheka tena, lakini lazima Wizara ya Fedha itumie uangalifu mkubwa katika kukopa ili Tanzania ijikute inarudi tena katika mazingira yaliyopelekea kuachwa kukopeshwa huko nyuma.

ARSENAL YASISITIZA DJOUROU NJE MSIMU WOTE!!


Klabu ya Arsenal maarufu kama Washika Bunduki wa Jiji la London wametoa taarifa inayosisitiza watamkosa Baki wake wa Kati Rais wa Uswiss kwa muda wote uliosalia kabla ya kumalizika kwa msimu. Johan Djourou alipata maumivu ya bega baada ya kugongana na Bakar Sagna katika mchezo wa Robo Fainal wa Kombe la FA dhidi ya Manchester United!!

MAN UTD NA INTER MILAN ZATINGA ROBO FAINAL CHAMPIONS LEAGUE!!




Klabu ya Manchester United ikiwa nyumbani katika Dimba la Old Trafford wamefanikiwa kutinga Robo Fainal ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuichakaza Marsseile kwa magoli 2-1!! Wakati Mabingwa Watetezi Inter Milan wamefanikiwa kuibuka kidedea mbele ya Bayern Munich kwa magoli 3-2 na kuendelea na mbio zao za kusaka Ubingwa!!

Wednesday, March 9, 2011

ARSENE WENGER ALIA NA MASSIMO BUSACCA!!



Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ameibuka mbogo na kumlaumu vikali Mwamuzi wa mchezo wao dhidi ya Barcelona, Massimo Busacca!! Kwa kifupi tu wale wasiomfahamu Busacca ni mwamuzi wa Uswiss tangu mwaka 1990 na alipata Beji ya FIFA mwaka 1999!! Lakini huyu ndiye aliyechezesha mchezo wa Fainali wa Ligi ya Mabingwa kati ya Barcelona na Manchester United!! Wenger na Rob Van Persie ambaye alizawadiwa kadi nyekundu kila mmoja amemlaumu Mwamuzi huyo kwa kusema alibadili mchezo baada ya kutoka kadi ya njano ya pili!!

RAIS KIKWETE SAFARINI ADDIS ABABA!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Machi 9, 2011, anaungana na marais wenzake wa Afrika waliopewa jukumu la kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Afrika Magharibi ya Ivory Coast, katika hatua za mwisho za jitihada za kujaribu kumaliza mgogoro huo.

Rais Kikwete na marais wenzake wanakutana mjini Addis Ababa, Ethiopia, katika jitihada mpya za kutafuta jawabu la mzozo huo uliolipuka mwishoni mwa mwaka jana kufuatia matokeo ya raundi ya pili ya uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo uliofanyika Novemba 28, 2011.

Katika mkutano huo wa siku mbili, marais hao wanatarajiwa kukabidhi ripoti yao kwa Kamati ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika (AU), ili kuuwezesha Umoja huo kuchukua uamuzi kamili wa jinsi ya kumaliza mgogoro huo.

Ripoti hiyo ni matokeo ya mikutano ya marais hao mjini Addis Ababa, huko Mauritania ambako walikutana mara mbili, na mjini Abidjan, Ivory Coast. Marais hao waliteuliwa na Kikao cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU katika mkutano wao wa Januari mwaka huu.

Rais Kikwete ameondoka nchini leo asubuhi kwenda Ethiopia kwa kikao hicho cha siku mbili ambako ataungana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Idriss Deby wa Chad, Rais Blaise Campaore wa Burkina Faso na Rais Mohamed Abdel Aziz ambaye ni mwenyekiti wa kundi hilo.

Wengine wanaotarajiwa kushiriki katika kikao hicho ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Bwana Jean Ping na wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Mataifa (UN).

Mzozo wa Ivory Coast ulianza baada ya taasisi mbili zinazosimamia uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo tofauti ya washindi wa raundi hiyo ya pili ya upigaji kura kati ya Mheshimiwa Laurent Gbagbo, aliyekuwa anatetea kiti chake na mpinzani wake mkuu, Mheshimiwa Alassane Quattara.

Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Quattara kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia tisa, lakini siku nne baadaye, Baraza la Katiba la nchi hiyo lilimtangaza Gbagbo kuwa mshindi kwa asilimia moja.

Baraza hilo lilimtangaza Gbagbo mshindi baada ya kuwa limefuta matokeo katika majimbo saba aliyokuwa ameshinda Quattara, kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiko ngome kuu yake ya kisiasa. Kwa kufuta matokeo katika majimbo hayo, Baraza lilimpunguzia Quattara kura 600,000.

Tokea wakati huo, viongozi hao wawili wote wamejitangaza marais na kila mmoja kuunda Serikali yake. Nchi hiyo sasa imetumbukia katika mgogoro kamili wa kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambako yamekuwepo mauaji ya watu na uharibifu mkubwa wa mali nchini humo.

IKULU YATEUA MNIKULU MPYA!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Shabani R. Gurumo kuwa Mnikulu (State House Comptroller).

Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam, leo, Jumatano, Machi 9, 2011 na Katibu Mkuu Kiongozi, Ndugu Phillemon Luhanjo inasema kuwa uteuzi huo unaanza mara moja.

Kabla ya uteuzi wake, Bwana Gurumo alikuwa Naibu Katibu wa Rais.

Bwana Gurumo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Marehemu Rajab Kianda ambaye alifariki dunia Februari 7, mwaka jana, 2010.

Mnikulu ndiye msimamizi mkuu na kiongozi wa shughuli zote za nyumbani za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na familia yake, na pia ndiye mkuu wa watumishi wote wanaohusika na shuguli hizo.

Aidha, Mnikulu ndiye msimamizi wa Ikulu na Ikulu Ndogo zote nchini na ndiye hukaribisha mabalozi wapya wanaoziwakilisha nchi zao katika Tanzania wanapokwenda Ikulu kukabidhi Hati za Utambilisho wao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

BARCELONA WADHIHIRISHA WAO NI WABABE MBELE YA ARSENAL!!






Barcelona wamefanikiwa kukata kidomodomo cha Arsenal baada ya kusitisha safari yao ya Ligi ya Mabingwa katika hatua ya mtoano!! Safari ya Arsenal ilifikia tamati Nou Camp!!

Monday, March 7, 2011

MAAMUZI YA UTATA YAENDELEA LIGI KUU ENGLAND!!




Mtafaruku uliozuka baada ya Jamie Carragher kumchezea rafu mbaya Luis Almeida Da Cunha Nani na kisha Refa Philp Dowd kutoa maamuzi ya kuchelewa na ambayo hayakuwa sahihi!! Maamuzi yanaendelea kuwa ni mabovu kila kukicha katika Ligi nchini England na kutishia kuharibu ubora wa Ligi hiyo!! Katika mchezo huo Man Utd walichakazwa magoli 3-1 na Liverpool!!