Tuesday, April 20, 2010

SERIKALI YA AWAMU YA NNE NA ELIMU!!!

Serikali ya Awamu ya Nne imefanikiwa kuwezesha asilimia 96 ya watoto wenye umri wa kwenda shule kuwa darasani kutoka asilimia 35 miaka sita iliyopita.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo leo jioni (19.4.10) Jijini New York katika sherehe ya chakula maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya kuzindua rasmi Mfuko wa Elimu Tanzania, Tanzania Education Fund.

“Mafanikio yetu ya kwanza yametokana na kuweza kuandikisha watoto kujiunga na elimu ya msingi na kuhakikisha kila mtoto anayetakiwa kuwa shule anakuwa darasani, miaka 6 iliyopita asilimia 35 ya watoto Tanzania ambao walitakiwa kuwa darasani walikuwa mitaani au wapo katika ajira”. Amewaambia waalikwa waliohudhuria chakula hicho cha jioni “sasa hivi ninapoongea nanyi, tumefanikiwa kuandikisha watoto shuleni kwa asilimia 96 na tumedhamiria kuwapeleka wote shuleni” Rais amesema.

Mfuko wa Elimu Tanzania, ni Shirika lisilo la Kiserikali(NGO) lililoanzishwa na marafiki wa Tanzania wa Kimarekani kwa kushirikiana na Serikali yaTanzania.

Kwa miaka minne sasa Serikali ya Awamu ya Nne imeweka kithara na kuelekeza nguvu zake katika kuhakikisha sekta ya elimu hapa nchini inaboreshwa na kuimarishwa. Kwa kuzingatia kithara hizo, bajeti ya sekta ya elimu imekuwa ikiongoza kwa ukubwa hapa nchini ili kuhakikisha kuwa malengo ya msingi ya Awamu ya Nne yanafanikiwa.

Malengo haya ya msingi ni “Kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume nchini Tanzania anapata elimu bora kuanzia elimu ya msingi, sekondari na hadi elimu ya juu” Rais amewaeleza marafiki wa Tanzania waliohudhuria chakula hicho.

Rais ameelezea mafanikio makubwa yaliyofikiwa ambapo mwaka 2000, Tanzania ilikuwa na shule za sekondari 927 na hadi kufikia mwaka 2009 shule hizo zimeongezeka kwa asilimia mia nne na kufikia idadi ya shule 4,102. Hivyo hivyo kiwango cha uandikishaji wanafunzi katika shule hizi za sekondari kimeongezeka kutoka 261,896 hadi kufikia milioni 1.46 katika kipindi hicho hicho.

Mafanikio mengine ni kwamba kati ya mwaka 2006 na 2009, jumla ya shule za sekondari 2,377 zimejengwa na hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 524,325 mwaka 2005, hadi kufikia wanafunzi milioni 1.6.

Hata hivyo Rais Kikwete amesema mafanikio yote haya yameleta changamoto mpya ambazo ni uhaba wa walimu, uhaba wa vitabu na vifaa vya kufundishia, uhaba wa vyumba vya maabara na nyumba za walimu.

Rais amewaambia waalikwa kuwa gharama za kutatua changamoto zote hizi zinazidi Dola za Kimarekani Bilioni 1.2 kwa miaka mitano, gharama ambazo kwa nchi maskini kama Tanzania ni mtihani ambao unahitaji ubunifu katika kuzitatua.

“Inahitajika ubunifu na ushirikiano katika kutatua changamoto hizi kutoka kwa marafiki na ndiyo maana tumekusanyika leo hapa”. Rais amewaambia waalikwa akiwemo mfanyibiashara Douglas Pitt ambaye amekuwa akisaidia Tanzania kimya kimya kwa zaidi ya miaka sita.

Katika sherehe hizo kabla ya chakula cha kuzindua mfuko wa Elimu Tanzania, Rais alimtangaza rasmi Bw. Douglas Pitt kuwa Balozi wa hiari wa Tanzania ambaye atakua na kazi ya kuitangaza Tanzania katika highly zake za kibiashara, utalii na elimu.

Bw. Douglas Pitt ni mdogo wake mcheza sinema maarufu wa Marekani Bw. Brad Pitt.

Rais Kikwete amekamilisha ziara yake ya kikazi nchini Marekani na anaondoka Jijini New York leo tarehe 20April, 2010 kurejea Dar-es-salaam.

No comments:

Post a Comment