Monday, April 19, 2010

CUF WALIA NA SHERIA YA WALEMAVU!!!

CUF – Chama cha Wananchi pamoja na kulipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha muswada wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, tunamsihi Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuharakisha kusaini muswada huo ili iwe sheria, lakini pia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu kuhakikisha kanuni zinaandaliwa mapema kwa ajili ya utekelezaji.

Muswada huo uliopitishwa Bungeni wiki iliyopita, umeridhiwa na Wabunge wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, na moja ya yaliyoridhiwa ni kuwepo kwa baraza la ushari litakalowashirikisha Watu wenye ulemavu na wadau wengine zikiwemo wizara za Serikali.

CUF – Chama cha Wananchi tunakila sababu ya kushinikiza kusainiwa muswada huo pia kuandaliwa kanuni zake haraka iwezekanavyo kama ilivyofanyika kwa muswada wa sheria ya gharama za uchaguzi, ili kuepusha yaliyotokea katika Sera ya Taifa ya Huduma ya Maendeleo kwa Watu wenye Ulemavu ambayo ilitolewa April 2004 na kuzinduliwa 2007 kwa kudandia maadhimisho ya Siku ya Watu wenye ulemavu duniani ambayo yameandaliwa na watu wenye ulemavu wenyewe.

Hiyo kama haitoshi hadi unaandaliwa muswada wa sheria ya haki za watu wenye ulemavu sera hiyo bado haijaandaliwa mkakati wa utekelezaji, jambo linalotia mashaka, hivyo ni budi maamuzi ya Bunge la Jamhuri ya kapewa thamani na uzito unaostahili kwa kutambua kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yana gusa kila binadamu alie hai kwani inatambulika kuwa “Hujafa Hujaumbika”.

CUF – Halikadhalika tunamtanabaisha Rais Jakaya Kikwete kuwa masuala ya Watu wenye Ulemavu ni mtambuka, na yanahusisha karibuni wizara zote za Serikali, hivyo basi hana budi kulitambua hili na kuhamisha masuala ya Watu wenye ulemavu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ili iwe rahisi kusimiwa na kufuatilia utekelezaji wake.

CUF – Tunawahimiza watu wenye ulemavu kuzitumia vyema haki zao na fursa zilizomo katika vyama vya siasa hususan chama mbadala Chama cha Wananchi – CUF, kwa kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea, na chama kinaahidi kuwa hakuna ubaguzi wowote, tutaheshimu uwezo wa mtu bila ya kujali maumbile yake.

No comments:

Post a Comment