Sunday, April 18, 2010

RAIS KIKWETE ALIVALIA NJUGA SUALA LA AFYA!!!

Changamoto Kubwa inayozikumba nchi zinazoendelea katika utoaji wa huduma za afya ni tatizo kuwa watu wa nchi hizi wanakabiliwa na maradhi mengi na wanaugua mara kwa mara.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo leo wakati alipokuwa anatoa mhadhara juu ya “Changamoto za Utoaji wa Huduma za Afya katika Nchi Zinazoendelea“ katika Chuo Kikuu cha Afya cha Weill Cornel Jijini New York.

“Afrika ina asilimia 11 tu ya idadi ya watu duniani lakini ina asilimia 24 ya mzigo wa maradhi duniani”, Rais amesema na kunukuu takwimu za shirika la Afya Duniani (WHO) ambazo zinaonesha kuwa kati ya vifo 10 vinavyotokea katika nchi tajiri, ni mtu mmoja tu ndiye anayekufa kutokana na magonjwa ya kuambukiza, wakati katika nchi maskini vifo sita kati ya kumi vinatokana na na maradhi ya kuambukiza.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa nchi maskini bado zinakabiliwa na maradhi ambayo yalishatokomezwa katika nchi zilizoendelea na kutoa mfano wa magonjwa kama malaria, kipindupindu, maradhi ya kuhara, typhoid na mengine mengi.

Rais Kikwete amewaeleza wanafunzi, wahadhiri na wageni waalikwa katika mhadhara huo kuwa, changamoto ingine inayozikabili nchi maskini ni uhaba wa wataalamu na huduma za afya ambazo ni pamoja na madawa na vitendea kazi, suala ambalo husababisha uchunguzi na matibabu kuwa magumu.

“Hata hivyo haya yote yanasababishwa na umaskini ambao umesababisha magonjwa makubwa kuwa mzigo na uwezo mdogo wa kukabiliana na maradhi” Rais amefafanua, pato la taifa la nchi zote Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mwaka 2008 lilikuwa dola za Kimarekani Bilioni 987.1, ambayo ni karibu na pato la taifa la nchi ya Korean ya Kusini ambalo lilikua Bilioni 992.0 na chini zaidi kuliko pato la Jiji la New York ambalo lilikua dola Trillion 1.4.

Hata hivyo pamoja na changamoto zote hizo Rais amesema, wananchi wa nchi zinazoendelea hawajakata tamaa na wanajitahidi kwa uwezo wao kuzikabili changamoto hizo na kujitahidi kuishi vyema, kwa kutengeneza sera, mipango na mazingira mazuri kulingana na hali halisi ya nchi zao.

Ameongeza kuwa kati ya jitihada hizo ni nchi hizi kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya sekta ya Afya ingawa hata hivyo siyo kubwa sana ya kuweza kutatua matatizo ya sekta nzima ya afya kwa vile nchi hizi hazina uwezo mkubwa.

Ametoa mfano wa Tanzania ambayo ina mpango wa Afya wa miaka kumi ambao unalenga katika kuongeza na kuboresha huduma za afya ambapo serikali imeadhimia kujenga vituo vya Afya Tanzania nchi nzima katika umbali usiozidi km 5 kutoka makazi ya wananchi, kuongeza juhudi za kupambana na maradhi kama malaria, ukimwi, TB na maradhi ya kuambukiza.

Serikali pia inajidhatiti katika kujenga uwezo wa kubaini, kupima na kutibu magonjwa makubwa nchini ili wagonjwa watibiwe nchini, kuongeza idadi na uwezo wa wataalamu.

No comments:

Post a Comment