Thursday, September 16, 2010

TAKUKURU YATAKIWA KUUNGWA MKONO KWENYE SHUGHULI ZAKE!!!

Katibu Mkuu Ikulu, Bwana Michael Mwanda amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Lindi, viongozi, Asasi Zisizo za Kiserikali pamoja na viongozi wa madhehebu ya dini mkoani humo, kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa vile jukumu la kupambana na rushwa ni la Watanzania wote.

“Jukumu la kupambana na rushwa ni letu sote na ndiyo maana kwa kutambua hilo, nipo hapa leo kuwaunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa. Napenda nitumie nafasi hii pia kuwahamasisha wananchi wote wa Mkoa wa Lindi pamoja na viongozi wenzangu kuwaunga mkono TAKUKURU katika mapambano haya mazito”, amesema.

Bwana Mwanda amebainisha hayo mjini Lindi 16 Septemba, 2010 akiwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa jengo la ofisi za TAKUKURU mkoani humo, iliyohudhuriwa pia na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na Asasi Zisizo za Kiserikali.

Katika hotuba yake, Bwana Mwanda amesema hatua ya TAKUKURU kujenga jengo la ofisi katika Mkoa wa Lindi, inatokana na dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Nne katika kuimarisha utawala bora na kuboresha utendaji wa kazi wa taasisi hiyo, kwa vile siku zote lengo la Serikali ni kupeleka huduma karibu na wananchi.

“…lengo la Serikali yetu siku zote limekuwa ni kupeleka huduma karibu na wananchi ili waweze kufanya shughuli zao za kimaendeleo kwa ufanisi na kuhakikisha kwamba kero ya rushwa inadhibitiwa vilivyo katika kila kona ya nchi yetu”, amebainisha Bwana Mwanda.

Amesema vita ya kuzuia na kupambana na rushwa ni kubwa inayohitaji umakini, moyo wa kujitolea na kujituma, na wakati mwingine kukubali lawama, hivyo Serikali imeona umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi ya watumishi wa TAKUKURU ili waweze kutoa huduma zilizo bora zaidi.

Bwana Mwanda amewatanabaisha viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kuwaelimisha waumini wao na hasa vijana kuhusu ubaya wa rushwa, na amewashauri kutumia nafasi waliyo nayo kutoa elimu ya maadili mema kwa waumini ili waepukane na maovu, hivyo kusaidia kwa kiwango kikubwa kujenga jamii adilifu na inayochukia vitendo vya rushwa.

Katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 31, 2010, Bwana Mwanda amewahimiza wananchi kuzingatia matakwa ya sheria zinazosimamia masuala ya rushwa katika uchaguzi, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo haugubikwi na vitendo vya rushwa.

Ili kuhakikisha kuwa TAKUKURU inapata mafanikio zaidi, Bwana Mwanda ameitaka Taasisi hiyo kuimarisha Kamati za Uadilifu zilizopo katika Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri za Wilaya, kuzishirikisha Asasi Zisizo za Kiserikali katika vita dhidi ya rushwa katika ngazi hizo, kuendelea kujenga uwezo wa watumishi wake, na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu rushwa.

No comments:

Post a Comment