Thursday, September 16, 2010

CUF NA MATOKEO YA UTAFITI YA SYNOVTE!!!

CUF – Chama cha Wananchi tumefarijika kwa taarifa iliyosahihi inayoelezea hali halisi ya utolewaji wa Habari za kampeni katika vyombo vya Habari, iliyoripotiwa na Meneja taasisi ya Synovate Bi. Jane Meela jana Jumanne, Septemba 14, jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ambayo imeripotiwa katika vyombo vya Habari imebainisha kwamba, katika utafiti wao wa pili Taasisi ya Synovate imegundua kuwa katika kampeni zinazoendelea Magazeti yameegemea kuripoti zaidi Chama cha Mapinduzi (CCM) na kufuatiwa na Chama cha Demokrasia Makini (CHADEMA) na kuviacha vyama vingine pasipo kupewa kipaumbele.

Taarifa hiyo imesema kuwa vyombo vya televisheni havikulalia upande wowote, taarifa zao wanazozitoa zinatoa kipaumbele kwa vyama mbalimbali (neutral) tofauti na vyombo vya magazeti, na isitoshe suala la amani limekuwa likizungumziwa zaidi katika kampeni zilizoripotiwa, halikadhalika Chama cha CHADEMA kilimepata kipaumbele mara baada ya kumtangaza mgombea wake wa Urais.

CUF – Chama cha Wananchi pamoja na kufarijika kwa ripoti hii ya Synovate ambayo inausahihi ndani yake, lakini pia tunamasikitiko kwa vyombo hivyo vya habari kwani pamoja na nia nzuri ya kuongozana na baadhi ya waandishi wao katika ziara za kampeni zetu za mgombea Urais na mgombea mwenza, lakini bado kipaumbele kimeelekezwa zaidi kwa wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia Makini (CHADEMA).

CUF – Tunawatanabaisha Watanzania kuwa dhamira ya makusudi inayofanywa na vyombo vingi vya habari (ukiacha vichache), hususani magazeti ni kujaribu kuonyesha kuwa upinzani uliopo katika uchaguzi mwaka huu kwa Tanzania Bara, ni baina ya CCM na CHADEMA, na kwa upande wa Zanzibar ni baina ya CCM na CUF, jambo ambalo halina ukweli kabisa.

CUF – Tunatambua kuwa harakati hizi hazikuanza leo, kwani waandishi walidiriki kulitamka hili bayana katika mikutano yetu na waandishi wa habari mapema mwaka jana 2009, kabla ya kuumbuliwa na matokeo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji zilizofanyika mwishoni mwa Oktoba mwaka jana, ambapo pamoja na taarifa halisi za matokeo hayo kutotangazwa na wizara ya TAMISEMI (kwa kuchelea kuumbuka), bado chama chetu kilifanya zizuri kuliko chama kingine chochote cha upinzani.

Ikiwa hata mwaka haujatimia tangu uchaguzi huo kufanyika, hayamkiniki kigezo kinachotumika na baadhi ya vyombo hivi vya habari kukipa kipaumbele chama ambacho kiliambulia mitaa saba tu, katika jiji hili la Dar es Salaam, na chama chetu kufanikiwa kuchukua mitaa 34, ambapo maeneo yaliyokuwa ni ngome zetu kuu ambayo ni wastani wa robo tatu wa wagombea wetu walienguliwa.

CUF – Tunavisihi vyombo vya Habari pamoja na kuifanyia kazi kamilifu ripoti ya Synovate, wazingatie maadili ya uandishi wa habari, jambo ambalo wamekuwa wakiliahidi na kujivuna nalo, hatupendi matukio ya mwaka 2005 ya wananchi wenye hasira kali kukosa imani na vyombo hivyo, yakajirudia katika uchaguzi huu.

HAKI SAWA KWA WOTE

No comments:

Post a Comment