Thursday, September 16, 2010

CUF WALAANI KUPIGWA KWA MWANDISHI KWENYE KAMPENI!!!

CUF – Chama cha Wananchi tumesikitishwa na kitendo cha mwandishi wa gazeti la Mwananchi Fredrick Katulanda, kuvamiwa na kushambuliwa na kikosi cha “janjaweed” wa Chama cha Mapinduzi wanatambulika kama “Green Guard” na kumjeruhi, katika kampeni za Ubunge katika jimbo la Sumve, Kijiji cha Nyambiti.

Walinzi hao walimshambulia mwandishi huyo na kumjeruhi sehemu za puani na mdomoni wakati wakimtaka yeye na wanataaluma wengine wa fani ya uandishi waondoke kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Jimbo hilo la Sumve, wilayani Kwimba.

CUF – Chama cha Wananchi tunalaani, kitendo hicho kuwa siyo cha kiungwana hata kidogo, licha ya kuhatarisha amani ya nchi lakini pia ni ukiukwaji mkubwa wa maadili na haki za binadamu cha kuwapiga waandishi wakiwa kazini.

CUF – Chama cha Wananchi tunatambua kuwa, vitendo hivi vimefanywa na Chama cha Mapinduzi, kutokana na mazoea ya kubebwa kwa kuripotiwa habari zao kwa kupambwa zaidi kuliko uhalisia, hivyo pindi waandishi wanapofuata maadili ya taaluma yao na kuripoti habari kama zilivyo, inakuwa nongwa kwa CCM, na kupanda jazba hatimaye kujichukulia sheria mikononi mwao.

CUF – Tunaviomba vyombo vyote vinavyohusika, kuwachukulia hatua kali Chama cha Mapinduzi, kwa uvunjifu huu wa amani, ukiukwaji wa maadili wakati wa kampeni na kwa vile ni vitendo vya jinai, tunalisihi jeshi la Polisi kuhakikisha wale wote waliohusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa Chama hicho.

CUF – Tunawatanabaisha Watanzania kuwa makini na chama hiki kinachoashiria uvunjivu wa amani iliyoasisiwa na wazee wetu, kwani hata ukiangalia baadhi ya mabango yao ya kampeni yanatoa vitisho kwenu wapiga kura ili msichague chama kingine iwapo kama mnataka amani, hii ina maana kuwa wapo tayari kuvunja amani iliyopo iwapo hawatachaguliwa.

HAKI SAWA KWA WOTE

No comments:

Post a Comment