Thursday, February 17, 2011

TAMKO LA CUF JUU YA MILIPUKO YA MABOMU!!

CUF – Chama cha Wananchi tunasikitishwa kwa tukio lililotekea kwa mara nyingine tena la milipuko ya mabomu katika kambi za Jeshi la Wananchi, awamu hii ikiwa ni kambi ya Gongolamboto jijini Dar es Salaam, ambapo taarifa za awali inakadiriwa watu zaidi ya 17 wamepoteza maisha yao na wengine zaidi ya 150 kujeruhiwa, lilotokea jana usiku kuanzia majira ya saa mbili na nusu.

Tukio hilo la ulipukaji wa mabomu ulioanzia ghala la kuhifadhia mabomu no. 5 na kusambaa katika maghala mengine 22 kati ya maghala 23 yaliyopo kambini hapo, na kusababisha mtafaruku mkubwa kwa wakazi wa maeneo ya jirani na kambi hiyo ambapo mamia ya wakazi hao wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani ( internal displaced people- IDP) na kuweka kambi za muda maeneo ya kambi ya kikosi cha kutuliza ghasia, uwanja wa Taifa, vituo vya polisi kama Buguruni na wengi wao kuhifadhiwa kwa ndugu na jamaa.

Tukio hili linachukua taswira ya tukio la jumapili ya tarehe 29 , Aprili mwaka 2009 ambapo, milipuko ya mabomu ilitokea katika ghala la kuhifadhia mabomu katika kikosi cha 671 KJ, Mbagala na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 20 na wengine wengi kupata ulemavu wa maisha, pamoja na uharibifu mkubwa wa majengo na maeneo ya makazi.

Pamoja na ahadi mbalimbali toka kwa Waziri mwenye dhamana ya ulinzi, Dr. Hussein Mwinyi ya kuhakikisha kuwa tukio kama hilo halitatokea tayari tukio tena kubwa zaidi ya lile la Mbagala limetokea, halikadhalika na kuonyesha ukaidi pale alipotakiwa kujiuzulu kutokana na uzembe uliofanyika ndani ya Wizara yake, ya kushindwa kuweka mazingira salama yasiyoweza kuleta madhara kwa wananchi.

CUF – Tunahuzunishwa na uzembe huu unaoendelea kujitokeza kwa makusudi na kuonyesha dharau ya kutothamini uhai wa raia wa nchi hii ambapo dhamana ya Jeshi la Ulinzi ni kulinda mipaka ya nchi na raia wake badala ya kuwawekea mazingia hatarishi ambayo yanasababisha maafa yakiwemo, kupoteza nguvu kazi ya taifa (ambayo ni vifo), kupoteza uwezo kuzalisha kutokana na ulemavu wanaoupata na kusababisha kuwa tegemezi.

Halikadhalika kuliingiza hasara Taifa ya ununuzi wa vifaa vingine vya kijeshi mbadala ya vilivyoangamia pasipo matumizi stahiki, jamii husika iliyoathiriwa kupoteza mali zao na kuchanganyikiwa kisaikolojia hadi kufikia kushindwa kuyamudu maisha yao kama ilivyokuwa awali, serikali na jamii kuingia gharama kubwa isiyotarajiwa ya kuhudumia waathirika wa maafa hayo ili hali nchi ikiwa imegubikwa na hali ngumu ya kimaisha ikiwemo madhara yanayochangiwa na ukosefu wa umeme wa uhakika, lakini pia serikali kuwajibika kuwalipa fidia wahanga hao, ambapo tukio hili likitokea bado kuna malalamiko ya waathirika wa mabomu ya Mbagala ya mwaka 2009 kuwa bado hawajalipwa fidia zao kama inavyostahiki.

CUF – Chama cha Wananchi tunaungana na Watanzania wote kwa msiba huu mzito wa kitaifa na kuwapa pole familia, ndugu na jamaa za wananchi waliopoteza maisha yao kutokana na milipuko ya mabomu hayo na kuwataka wawe na subira katika kipindi hiki cha majonzi, na kumuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amin!!!!

Halikadhalika tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu wale wote waliomajeruhi awaponyeshe haraka, na pia tunawasihi watanzania popote pale tulipo kujitolea kwa hali na mali kuwasaidia waathirika hawa kwa kila tunachokimudu ili angalau kuwapunguzia makali ya madhara waliyoyapata.

CUF – Kwa mara nyingine tena tunamtaka Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Dk. Hussein Mwinyi na Mkuu wa JWTZ, Mheshimiwa Davis Mwamunyange, kuwajibika kwa kujiuzulu mara moja kutokana na ukaidi na kushindwa kudhibiti madhara yaliyojitokeza siku za nyuma yasijitokeza tena, tunamsihi Waziri Mwinyi kulinda heshima yake kwa kufuata nyayo za baba yake Mzee Ali Hassan Mwinyi alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alipojiuzulu kutokana sakata la mauaji mkoani Shinyanga.

CUF – Tunamtaka Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwahakikishia wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuishi bila hofu kutokana na matukio yanayoendelea kujitokeza ya milipuko katika kambi za jeshi, ili hali jiji hili likiwa limezungukwa na kambi mbalimbali za jeshi katika kila upande, Kigamboni, Lugalo, Mgulani, Upanga, Mabibo, Mbweni na kwengineko.

No comments:

Post a Comment