Monday, October 11, 2010

MATOKEO YA SYNOVATE YASHUKIWA!!!

CUF – Chama cha Wananchi tumesikitishwa na taarifa ya utafiti wa taasisi ya Synovate iliyotolewa jana Oktoba 10, jijini Dar es Salaam na kuripotiwa na vyombo vya habari leo hii namna inavyojichanganya, kwani idadi ya wanaomkubali Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi Jakaya Kikwete ni wengi kuliko vyama vingine, wakati huo huo wanaokiri kutoridhishwa na huduma zake ni wengi.

Kwa mujibu wa vyombo vya Habari, ripoti hiyo inaonyesha Dkt. Jakaya Kikwete anakubalika kwa asilimia 61, Dkt. Willbrod Slaa ana asilimia 16 na Prof. Ibrahim Lipumba ana asilimia 5, lakini wakati huo huo inaeleza ripoti hiyo kuwa katika utendaji wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete watu wengi waliohojiwa hawakuridhika na huduma zinazotolewa katika upatikanaji wa ajira (84%), bei za vyakula (72%), maji safi ya kunywa (49%), afya(48%), mapambano dhidi ya rushwa(61%) na mapambano dhidi ya kuondoa umasikini(86%).

Katika ripoti hiyo hiyo, pamoja na kuonyesha wananchi wasivyoridhishwa na utendaji wa serikali hiyo ya Jakaya Kikwete, lakini bado wana imani na Rais Kikwete kwa asilimia 84, Baraza la Mawaziri (68%), Jeshi la Polisi (45%), Baraza la Mitihani (50%), mahakama (52), taasisi za huduma za afya (50%), TAKUKURU (46%) na vyama vya upinzani (48%).

Kwa upande wa elimu ya msingi ripoti inaonyesha kuwa wanaoridhika na utolewaji bora wa elimu ni asilimia 82, na kwa elimu ya sekondari wanaoridhika na utolewaji wa elimu bora ni asilimia 77.

CUF – Chama cha Wananchi tunasema iwapo kama ni kweli taarifa iliyoripotiwa ndivyo ilivyo tunasikitishwa namna taaluma ya utafiti inavyotumika vibaya, kwani hayamkiniki mtu mwenye akili timamu hata kama hakwenda shule, hata awe mtoto wako nyumbani, wakati akijua fika, tena kwa uhakika kwamba wewe umeshindwa kumpatia huduma muhimu (kama ripoti inavyoonyesha) na akawa bado eti ana imani na wewe na watendaji wako, huu ni uzushi mtupu.

CUF – Chama cha Wananchi tunaitaka taasisi ya Syonovate iwaombe radhi watanzania, kwani ripoti yao inaonyesha kuwa, wananchi wa nchi hii bado ni mbumbumbu wa kumpenda mtu kwa sura yake na wakaendelea kuwa na imani nae hata kama wanatambua fika ameshindwa kuwapatia huduma muhimu, huku ni kuwadhalilisha Watanzania na kazi kubwa inayofanywa na vyama vya upinzani, taasisi zisizo za kiserikali na vyombo vya habari juu ya kuelimisha umma.

CUF – Tunawatahadharisha Watanzania kuwa makini katika kipindi hiki cha uchaguzi, kwani taasisi mamluki zitatumia taaluma zao kuwapotosha na kuwavunja moyo mliokuwa nao wakukataa ufisadi na dhuluma inayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi dhidi ya mali asili na mapato ya nchi, ili siku ya uchaguzi Oktoba 31, wananchi msijitokeze kwa wingi kwa kudhani kuwa CCM bado inakubalika, TUNAWASIHI WANANCHI WA TANZANIA WALIOJIANDIKISHA KUPIGA KURA, JITOKEZENI KWA WINGI SIKU YA KUPIGA KURA NA MFANYE MAAMUZI SAHIHI YA KULETA MABADILIKO.